Hesabu mpya za Fei Toto Azam, amtaja Ibenge

KIUNGO mahiri wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameweka wazi malengo yake ya msimu huu akisema anataka kufunga mabao 15, huku akimpa maua kocha Florente Ibenge.

Fei Toto ambaye aliyewahi kuichezea Yanga huu ni msimu wake wa tatu Azam FC akiwa ameshafunga mabao mawili kwenye ligi, huku msimu uliopita aliibuka kinara wa asisti akiwa nazo 13 sambamba na kufunga mabao manne. Kabla ya hapo, msimu wa kwanza ndani ya Azam 2023-2024 alifunga mabao 19 na asisti saba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto amesema, msimu huu hana mpango kabisa na rekodi za asisti huku akitaka kufunga mabao zaidi.

Amesema mabao 15 kwake sio machache ingawa ameshawahi kufunga zaidi ya hayo, hivyo kila msimu huwa unakuja na mipango yake na huo ndio alionao kwa sasa.

FEI 02

“Msimu huu nataka kufunga mabao 15, na sasa nimeshatia kambani mawili. Kwa hiyo mzigo unazidi kupungua taratibu. Kama mambo yakienda vyema, basi yanaweza kuzidi. Kwa sasa napambania kufika hapo.

“Nafasi yangu uwanjani kwa sasa nacheza namba 10 na hata kocha anavyonitumia ni tofauti na msimu uliomalizika. Kuna majukumu yamepungua,” alisema Fei Toto.

FEI 01

Fei Toto amesema, uwepo wa kocha mkubwa kama Ibenge ndani ya Azam unaongeza kitu kikubwa kwa timu, lakini hata kwake anaamini sana kwamba kuna vitu vitaongezeka.

“Makocha wote ni wazuri, ila wanatofautiana na sasa tuna Ibenge, kiukweli ni kocha mwenye mbinu nzuri anayeamini katika juhudi za mchezaji kuanzia mazoezini.

“Naiona Azam ya tofauti msimu huu kama kwa pamoja tutaungana kuhakikisha tunaipeleka timu mbali hasa katika michuano ya kimataifa na ya ndani na huo uwezo tunao,” alisema mchezaji huyo.

Huu ukiwa ni msimu wa tatu Fei Toto ndani ya Azam, amefunga mabao 25 kwenye Ligi Kuu Bara na asisti 20, huku ikielezwa katika mkataba wake mpya aliosaini hadi 2027 kuna kipengele cha bonasi endapo akifunga mabao mengi zaidi.