NISHATI YAWASILISHA MIPANGO YA KIMKAKATI KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050

…………………………..

📌 Ni katika kikao kazi na Tume ya Taifa ya Mipango.

📌Mradi wa usafirishaji umeme Chalinze–Dodoma ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele kufanikisha Dira 2050,

📌Wizara ya Nishati na Tume ya Mipango kushirikiana kwa karibu kusimamia miradi ya Nishati kufanikisha malengo ya Dira 2050.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amekutana na wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango wakiongozwa na Naibu Katibu Mtendaji – Menejimenti ya Utendaji na Tathmini, Dkt. Linda  Ezekiel kwa lengo la kujadili namna ambavyo Wizara na Taasisi zake zimejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati ya nishati inayochangia katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Msingi wa kikao hicho umetokana na  Sekta ya Nishati kuainishwa katika Dira 2050 kuwa ni moja ya  vichocheo vitano vitakavyoongeza kasi ya kufikia malengo ya Dira hiyo, ikielezwa kuwa Nishati ya uhakika ni nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha viwango vya maisha kwa kutoa fursa za ajira kwa maendeleo endelevu katika jamii.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma na  kuhusisha Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, 

Mha. Mramba amesema pande hizo mbili zimejipanga kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa miradi ya nishati ili kuhakikisha kuwa  inalingana na vipaumbele vya kitaifa vya maendeleo. 

“Wizara ya Nishati inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya nishati ukiwemo mradi wa  kusafirisha umeme wa kV 400 wa Chalinze–Dodoma, ambao unatarajiwa kukamilika Juni 2026. Huu ni moja ya miradi  itakayoleta chachu ya kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Katavi, Kigoma na maeneo mengine ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa umeme thabiti.” Amesema Mhandisi Mramba

Amesema kukamilika kwa miradi ya kimkakati ya umeme kutawezesha kutimiza moja ya shabaha katika Dira 2050 ambayo inaelekeza kuwa matumizi ya umeme yanapaswa kuongezeka na kufikia wastani wa Kwh 3,000 kwa kila mtu kwa mwaka.

“Tunataka kuwa Taifa lenye nishati ya uhakika, nafuu na safi kwa watanzania wote,  ili kutimiza lengo hili Serikali inawakaribisha wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya nishati  kwa kuwa mafanikio ya sekta hii yanategemea ushirikiano wa wadau wote. ” Amesisitiza Mhandisi Mramba

Katika kikao hicho, Wizara pia iliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Gesi Asilia na Mafuta,  Nishati Safi ya Kupikia, Umeme na Nishati Mbadala.

Kwa upande wake, Dkt. Linda  Ezekiel kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na Tume hiyo akisisitiza kuwa mwelekeo wa miradi iliyoainishwa katika kikao hicho inaendana na malengo ya Dira 2050.

Amesema Tume itaendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha inachangia moja kwa moja katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, kuboresha ustawi wa wananchi, na kulinda mazingira.

“DIRA ya 2050 inalenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi. Sekta ya Nishati ni mhimili wa kufanikisha hayo yote, tunapongeza jitihada za Wizara ya Nishati katika kuhakikisha nishati inakuwa injini ya maendeleo.” Ameeleza Dkt. Ezekiel

Kupitia kikao hicho, Wizara ya Nishati na Tume ya Taifa ya Mipango zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia miradi yote inayogusa Sekta ya Nishati ili kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya  DIRA ya Maendeleo 2050 kwa ufanisi.