MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich imehusishwa na mpango wa kufanya shambulizi la kushtukiza la kumsajili beki wa Crystal Palace, Marc Guehi.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye ni nahodha wa Palace, aliongoza timu hiyo yenye maskani yake kusini mwa London kutwaa Kombe la FA kwa mara ya kwanza katika kihistoria yao, msimu uliopita.
Kiwango kimezivutia klabu nyingi za ndani na nje ya England kutamani kumsajili na sasa, kwa mujibu wa taarifa kutoka, Sky Sports, Bayern imejiunga kwenye orodha ya timu zinazomtaka beki huyo.
Inaelezwa Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern, Max Eberl, ni shabiki mkubwa wa Guehi na angependa kuona akitua Munich ili acheze sambamba na Harry Kane, ambaye ni mchezaji mwenzake katika kikosi cha timu ya taifa ya England.
Mkataba wa Guehi na Palace unamalizika mwishoni mwa msimu huu na licha ya klabu hiyo kutaka kumuongezea, mwenyewe haonekani kua na nia ya kuendelea kusalia.
Katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Guehi alihusishwa sana na uhamisho kwenda kwa mabingwa wa Ligi Kuu England, Liverpool, lakini mpango huo ulivunjika dakika za mwisho baada ya kocha wa Palace, Oliver Glasner, kutishia kujiuzulu ikiwa atauzwa kwa sababu klabu haikuwa na mbadala wake kwa wakati huo.
Hata hivyo, inaaminika Liverpool bado haijakata tamaa na huenda ikarudi tena kwa nguvu zote kutaka kumsajili beki huyo Januari mwakani.
Timu nyingine kubwa Ulaya inayohusishwa naye ni Real Madrid ambayo imekuwa ikivutiwa sana na Guehi na inadaiwa hata mchezaji mwenyewe anapendelea zaidi kujiunga na timu hiyo.
Uwezekano wa uhamisho huo kwenda Hispania unachagizwa zaidi na sheria maalum ya usajili wa wachezaji katika nchi hiyo.
Guehi alizaliwa Ivory Coast na anamiliki pasipoti ya Kiafrika ya nchi hiyo kupitia uraia wa baba yake jambo linaweza kumruhusu kusajiliwa na Madrid kama raia wa Hispania kupitia makubaliano ya Cotonou (Cotonou Agreement), mkataba unaoruhusu wachezaji kutoka nchi washirika wa Afrika kuhesabiwa kama raia wa Hispania.