Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhe. Balozi Ombeni Sefue, amesema kuwa Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga (EACOP) ni miongoni mwa miradi bora zaidi duniani kwa kuzingatia utu, haki za wananchi na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Balozi Sefue amesema mradi huo umejikita katika kuhakikisha wananchi waliopitiwa na bomba wanapata fidia stahiki, ajira, na manufaa mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.
“Haikuwa rahisi kwa Tanzania kuupata huu mradi, kwa kuwa kulikuwa na njia nyingi zilizokuwa zikifikiriwa kupitisha bomba. Mafanikio ya kwanza ni kuupata mradi huu, na sasa tumeendelea kunufaika zaidi kupitia ongezeko la pato la taifa, fidia nzuri kwa wananchi, pamoja na kandarasi nyingi zinazotekelezwa na kampuni za kizalendo,” amesema Balozi Sefue.
Ameongeza kuwa hatua iliyofikiwa hivi sasa ni ya kukamilisha ujenzi, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya viongozi na wananchi ili kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa wakati.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhe. Balozi Ombeni Sefue akizungumza