Rais Mwinyi ataja kinachoshusha uzalishaji wa karafuu Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema Serikali imebaini kupungua kwa uzalishaji wa zao la karafuu kutokana na wakulima kuacha kushughulikia mashamba kwa sababu ya kudhulumiwa unapofika msimu wa kilimo.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 7, 2025, wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa hati za mashamba ya Serikali yanayotumika kwa kilimo, hususan karafuu, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema uzalishaji wa karafuu upo chini ya tani 10 kwa mwaka ikilinganishwa na tani 100,000 zinazozalishwa Indonesia, ambao wana mazingira kama ya Zanzibar.

“Tulitafakari tukaona kuna changamoto za utunzaji, watu hawatunzi mashamba kwa sababu hawaoni tija. Maana ukifika msimu, wanadhulumiwa, kwa hiyo wakaamua kuyatelekeza,” amesema Dk Mwinyi.

Baada ya kukabidhi hati hizo, Dk Mwinyi amewataka waendelee kuyashughulikia mashamba hayo kwani hakutakuwa na dhuluma, ili kilimo cha karafuu kiwe na tija, kuinua uchumi wao na nchi kwa ujumla.

Amesema lengo la Serikali ni kuona uzalishaji unaongezeka zaidi ya mara mbili ya sasa.

“Tutahakikisha tunapanda miche, tutawapa mikopo isiyokuwa na riba, naamini baada ya muda mfupi tutaweza kufikia uzalishaji wa tani 20 kwa mwaka na zaidi,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, utolewaji wa hati hizo utaondoa migogoro ya mipaka na kuwapa wakulima uhakika wa umiliki.

Amesema mbali na uamuzi wa ugawaji wa hati, pia Serikali kupitia Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC) limeanzisha mfumo wa ununuzi wa karafuu kidijitali na kuachana na utaratibu wa kusafirisha zao hilo hadi kwenye vituo vya kuuzia.

“Wakulima wanafuatwa kwenye maeneo yao kununua ili kuwaepushia usafirishaji, na ZSTC imeanza kutoa bima kwa wachumaji wanapopata ajali na wanaendelea kutoa miche ya mikarafuu bure,” amesema.

Pamoja na hayo, amesema itaendelea kumlipa mkulima asilimia 80 ya mauzo yanayopatikana. Itakumbukwa ZSTC ndio ananunua karafuu kwa mkulima na kuuza, kwa hiyo mkulima anapata asilimia 80 ya kinachopatikana kwa kila kilo.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Thabit, amesema kumekuwapo na usimamizi tofauti wa mashamba hayo huku yakiibua changamoto lukuki.

Amesema walifanya uhakiki na kubaini kuna mashamba 8,215 yalitolewa na Serikali baada ya Mapinduzi ambapo kila mwananchi alipewa ekari tatu.

Amesema utaratibu wa kutoa hati za mashamba ya Serikali umeshaanza kwa Unguja, ambapo tayari zimeshatolewa hati 112, na wameanza kutoa kwa Pemba ambapo wameanza na hati 30.

Hata hivyo, amesema ili kuweka uendelevu wa mashamba hayo, wanaomba kitengo cha ekari kiimarishwe na watendaji waliokuwa wanasimamia mashamba hayo wakati yakiwa chini ya Wizara ya Kilimo, wahamishiwe katika Wizara ya Ardhi waendelee kuyasimamia kwa sababu wana uelewa mpana.

Pia, amesema katika uhakiki walibaini kuna watu wanamiliki zaidi ya ekari tisa, ambapo ni kinyume na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1992, kifungu cha 44, ambacho kinataka miliki ziwe ekari tatu.

“Aliyeendeleza nusu sehemu nyingine akashindwa na wanakwenda kinyume na masharti, tunaomba anyang’anywe, wapewe wengine waendeleze,” amesema.

Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Rahma Kassim Ali, amesema kazi hiyo wataisimamia kwa ukaribu licha ya changamoto nyingi.

“Mashamba ni mengi, zaidi ya 8,000, tunataka tuyapime haraka kila mmoja apate hati yake kwa kuendeleza kilimo,” amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk, amesema jambo hilo litapunguza migogoro, na hivyo wakulima na wananchi watamkumbuka Dk Mwinyi kwa hatua hiyo.

Baadhi ya wakulima waliopewa hati hizo, akiwemo Halima Khamis Ali, amesema walikuwa wakihangaikia mikarafuu lakini wakati wa mavuno hawaambulii kitu.

“Ulikuwa unapanda, unalinda, ila ikifika wakati wa kuvuna wanakuja watu wengine kuchukua. Tunapongeza hatua hii, kwa kweli itatusaidia wakulima wengi,” amesema Halima.