Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa taarifa ya mabadiliko ya idadi ya wapigakura, ambapo sasa watakuwa 37,647,235 badala ya 37,655,559 iliyokuwa imetangazwa awali.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.53 kutoka idadi ya wapigakura 29,754,699 waliokuwa kwenye Daftari la Wapigakura mwaka 2020.
Mabadiliko hayo yamekuja baada ya INEC kupokea taarifa kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuhusu mabadiliko ya takwimu za idadi ya wapigakura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya INEC iliyotolewa leo Oktoba 7, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, orodha hiyo inaonesha wapigakura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na 996,303 wapo Tanzania Zanzibar.
Kati yao, wanawake ni 18,950,801, sawa na asilimia 50.34, na wanaume ni 18,696,439, sawa na asilimia 49.66.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa jumla ya vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kwenye uchaguzi mkuu ni 99,895, badala ya 99,911 iliyotangazwa awali, baada ya ZEC kufanya marekebisho ya vituo vya kupigia kura.
Katika mgawanyo huo, Tanzania Bara itakuwa na vituo 97,348 na Tanzania Zanzibar vitakuwa na 2,547.
Idadi hiyo ya vituo 99,895 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.47 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu 2020.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uandikishaji wa wapigakura kwa upande wa Tanzania Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge, unazingatia sheria inayohusu uandikishaji wa wapigakura kwa ajili ya uchaguzi katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na mabadiliko yatakayofaa.
“Daftari la wapigakura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar litakuwa sehemu ya Daftari la Wapigakura la Tume ya Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge upande wa Tanzania Zanzibar,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.