Serikali kuleta sheria tiba ya kurejesha ujana

Dar es Salaam. Serikali imesema iko mbioni kukamilisha utengenezaji wa sheria ya upandikizaji viungo itakayofungua milango kwa huduma mbalimbali ikiwemo kurejesha ngozi, nywele maarufu tiba urejeshaji ‘Regeneretive Medicine’.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mwananchi kuchapisha habari kuhusu huduma mpya ya tiba ya urejeshaji inayohusisha matumizi ya seli shina za mwili wa binadamu, ambayo husaidia mwili kujitibu kwa kutumia seli zake asilia pasipo upasuaji.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Oktoba 8, 2025 Mkurugenzi Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea kuhusu tiba za urejeshaji amesema kinachofanyika sasa huduma za kibobezi za upasuaji rekebishi, zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuna wataalamu waliosomea na wagonjwa wengi wameshanufaika.

“Wizara inaendelea kukamilisha sheria ya upandikizaji viungo ambayo itafungua milango kwa huduma za upandikizaji viungo ikiwemo urejeshaji nywele, ngozi, meno na nyinginezo. Sheria hii itakamilika Bunge lijalo,” amesema Nyembea.

Wizara  ya Afya, inaandaa muswada wa sheria ya uvunaji, usimamizi na utunzaji wa viungo vya ndani vya binadamu, itakayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo mbalimbali ikiwa ni pamoja na figo, maini, magoti, moyo  na mapafu.

Muswada huo pia unalenga kuvuna viungo kwa watu waliofariki na kuridhia viungo vyao vitumike kwa watu wenye uhitaji.

Sheria hiyo inakuja kukiwa na uhitaji mkubwa wa huduma hizo nchini Tanzania kutokana na mabadiliko ya mtazamo wa jamii, ambapo watu wengi sasa wanathamini zaidi urembo, afya ya ngozi na mwonekano wa ujana.

“Siku hizi ngozi ni kila kitu. Ukiwa na ngozi safi na laini, unaonekana kijana hata kama una miaka 40. Mimi siwezi kutoka bila kupaka mafuta ya collagen, nataka ngozi yangu iendelee kung’aa,” amesema Angela Mwisi (46) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Mkazi wa Msasani Joyce Mfilinge, amesema kuwa anapenda kutumia vipodozi vilivyotengenezwa kwa collagen na bidhaa za kupambana na uzee ili kuwa na ngozi laini, yenye kung’aa na kuonekana mchanga zaidi, hasa kutokana na ukweli kwamba mwili wake huwa unatoka vipele vinavyoacha alama.

Hata hivyo uhitaji huo unakuja sambamba na jamii kuathiriwa na bidhaa bandia za ngozi, wengi waliopata madhara kutoka kwa krimu zenye kemikali kali sasa wanatafuta tiba za urejeshaji wa ngozi.

“Mwaka 2021 nilitumia kipodozi kikaniharibu ngozi, naifahamu tiba ya urejeshaji niliipata Afrika Kusini na nikafanikiwa kurejesha ngozi yangu ya awali. Sio kila mwanamke anayetaka ngozi laini anataka kuonekana mdogo, wengine tunataka tu afya ya ngozi,” amesema mkazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Grace (52).

Pia wapo waliopata matatizo ya upara yanayochochewa na msongo wa mawazo, mabadiliko ya homoni, au matumizi ya dawa. Wanaume na wanawake wote sasa wanatafuta suluhisho la kudumu.

Hali hiyo pia inatajwa kutokana na kuongezeka kwa watu wa kipato cha kati zaidi ya miaka 10 iliyopita, huduma hizi zilikuwa nadra na ghali, lakini hivi sasa kliniki binafsi zinazidi kuibuka Dar es Salaam, Arusha na Mwanza zikitoa huduma hizo.

Aidha madaktari ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitoa tiba za upasuaji wa kurekebisha maumbile, wamesema uhitaji kwa sasa ni mkubwa lakini wengi wanashindwa kumudu gharama.

Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Erick Muhumba amesema uhitaji ni mkubwa huku akitaja changamoto ni gharama.

“Wanaohitaji tiba rekebishi ya maumbile yao, kupunguza au kuongeza na kupandikiza nywele wapo wengi. Kuna matibabu bado hatujaanza kuyatoa, hata hivyo wengi wanakuja, wanaulizia lakini wanashindwa kulipa wanaondoka na wanaolipa ni wachache tunawahudumia,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Daktari wa masuala ya urembo anayetoa huduma ya tiba ya urejeshaji Nairobi nchini Kenya, Arshni Malde alisema tiba hiyo imeanza kuvutia watu wengi kutokana na matokeo yake ya haraka na gharama nafuu ikilinganishwa na upasuaji wa plastiki au vipodozi vyenye collagen.