MGOMBEA Udiwani wa Kata ya Mabibo, wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam, kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ashura Mohammed Seg’ondo, amewataka wananchi katika kata hiyo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 mwaka huu kumpigia kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na yeye kwa nafasi ya udiwani ili kuwaletea maendeleo ya haraka.
Aidha amewataka kumchagua Mgombea Ubunge kwa tiketi ya CCM katikaJimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo hali itakayo harakisha maendeleo katika kata hiyo.
Akihutubia mkutano wa kampeni katika kata hiyo, Ashura alisema akichaguliwa kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha anasimamia kikamilifu ujenzi wa miundo mbinu.
“Miundombinu nimeigawanya katika sehemu mbili. Barabara kuu na barabara za ndani. Katika Mtaa wa Jitegemee mkandarasi tayari anaendelea na ujenzi wa Barabara ya Binti Kayenga. Nami kwa kushirikiana na nyie nitahakikisha kwa ujasiri wangu mkubwa kwa nguvu zangu zote mkandarasi afanye kazi kwa haraka kukamilisha ujenzi,”ameeleza Ashura.
Amebainisha, Kata ya Mabibo, imejaaliwa viwanda vikubwa hivyo kwa kushirikiana na viongozi atahakikisha kwa asilimia kubwa wakazi wa kata hiyo watananufaika na ajira.
“Pia katika sekta ya michezo nitahakikisha tunashirikiana vyema ili iwe fursa ya ajira kwa sababu Kata ya Mabibo ni ni kitovu cha mchezo wa ngumi. Bondia Mfaume Mfaume anatoka katika kata hiii,”ameeleza.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri , Ashura ameeleza atahakikisha inawasikia walengwa.
“Mikopo inakuja lakini haiwanufaishi walengwa. Nikichaguliwa nitahakikisha mikopo hii inawafikia walengwa. Inawanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kausha damu itakuwa baibai,”ameeleza mgombea huyo.
Amesema atafanya jitihada kuleta walimu wa vikoba kutoa elimu kwa wananchi katika kata hiyo ili viinue uchumi hasa wawanawake.
![]() |