Viongozi wa Airtel Tanzania Watembelea Kituo cha Huduma kwa Wateja Kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, uongozi wa Airtel Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Charles Kamoto, pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Bi. Beatrice Singano, wametembelea kituo cha huduma kwa wateja cha Airtel jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo imelenga kuwatambua na kuwapongeza watoa huduma kwa wateja kwa kazi yao muhimu ya kila siku katika kuhakikisha huduma bora na zenye ubunifu zinawafikia wateja kote nchini.

Wakati wa ziara hiyo, viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza na watoa huduma na kushiriki katika kupokea simu kutoka kwa wateja waliokuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali za mawasiliano na huduma. Hatua hiyo iliwapa nafasi ya kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu mahitaji na changamoto za wateja, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Airtel ya kuboresha huduma na kuimarisha falsafa yake ya “Mteja Kwanza.”
Aidha, Bw. Kamoto alitumia fursa hiyo kuwazawadia wafanyakazi bora wa mwezi Septemba wakiwemo Arapha Joseph, Rashidi Msuya na Syliakus Kaiza, kwa kutambua mchango wao katika kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku za kituo hicho.
Tuzo hizo zilitolewa kama ishara ya kuthamini bidii, weledi na kujituma kwao katika kuhakikisha huduma bora zinawafikia wateja kwa wakati.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bw. Kamoto aliipongeza timu ya huduma kwa wateja kwa kujituma na kujitoa kwao katika kuhudumia wateja, akisisitiza kuwa mafanikio ya Airtel yamejengwa juu ya ubora wa huduma na uhusiano mzuri kati ya wateja na watoa huduma. Alitoa wito kwa timu hiyo kuendelea kutoa huduma zenye ubunifu, ufanisi na huruma kwa wateja wote.