Wanazuoni wahimiza amani, haki, wajibu kuelekea uchaguzi

Dar es Salaam. Umoja wa wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, umehimiza kudumishwa amani, haki na uadilifu kwa kila Mtanzania kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa wanazuoni hao, Taifa lenye ustawi linajengwa kwa haki na huruma na hakuna nguvu inayoweza kuvunja Taifa linaposhikilia mshikamano wake.

Wito wa wanazuoni hao, ulitolewa jana Jumatatu, Oktoba 6, 2025 kupitia waraka maalumu uliotiwa saini na kugongwa muhuri na umoja huo.

Katika waraka huo, wameeleza kuwa, kila Mtanzania aendelee kutumia haki zake za Kikatiba bila hofu, huku amani ikizingatiwa kwa kuwa ndio msingi wa kila kitu.

“Kwa kuwa viongozi wa dini, hatuhamasishi kuchagua mgombea fulani au chama fulani, badala yake tunaheshimu Taifa letu, tunalinda amani na ustawi wake kwa kuhimiza ushiriki salama na wa amani kwa wananchi wote,” wameeleza.

Katika waraka huo, umoja huo umeeleza kuwa, uchaguzi huo ni fursa ya kuonesha uwajibikaji na ujasiri wa nchi katika kuilinda Katiba.

Pia, wameeleza kila kura ni kipimo cha uhuru na uchambuzi wa matumaini ya Taifa kuendelea kuwa na amani, ustawi na mshikamano.

“Tusiingize propaganda, chuki, wala ubaguzi wowote wa kisiasa, kidini au kikabila, kuvunja umoja wetu na kuharibu maendeleo ya Taifa letu,” wameeleza kupitia waraka huo.

Wanazuoni hao, wametolea mfano wa nchi za Malaysia, Indonesia na Morocco zilizoonesha thamani ya uchaguzi huru na wa haki.

Wameeleza kuwa, viongozi wa dini na kijamii wametoa wito wa amani na uwazi wakati wa kampeni, huku nchi hizo zikijenga mifumo thabiti ya kulinda haki za wafuasi wa dini zote.

“Hakika amani ni neema kubwa zaidi baada ya imani. Ni upofu wa kimaono kudhani kuwa, Taifa linaweza kufikia maendeleo ya kweli, bila kuhakikisha kwanza wananchi wake wanalindwa dhidi ya vurugu na hofu,” wameeleza.

Kuhusu mipango mikubwa ya kiuchumi na kijamii, wameeleza kuwa, haina maana yoyote ikiwa inatekelezwa katika mazingira yenye migogoro, ukosefu wa haki na utulivu dhaifu.

Pia, wameomba kuwe na ahadi ya dhati ili kulinda amani na utulivu wa Taifa, kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi, kwa kuwa jamii inahitaji watu wa uamuzi mwema ambao hawatafanya vurugu pale tofauti zinapojitokeza.

“Tunawahimiza wagombea wote, bila kujali vyama vyao, watambue kuwa kiongozi wa kuaminiwa ni yule mwenye dhamira njema ya kulinda na kudumisha utulivu wa Taifa,” wameeleza katika waraka huo.

Kwa mujibu wa waraka wa wanazuoni hao, kipindi chote cha kampeni, ahadi za wagombea ziwe za kweli na hatua zao ziakisi uwazi na nia walizonazo.

Kupitia waraka huo, umoja huo umeeleza kuwa, vyombo vyote vinavyosimamia mchakato wa uchaguzi vinapaswa kuongozwa na misingi ya haki na uadilifu.

Wameeleza kuwa, hatua zote kuanzia usajili wa wapigakura, utoaji wa fomu, upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo, zitekelezwe kwa uwazi, usawa na bila upendeleo.

“Hili ndilo jukumu la pamoja na uwekezaji wa Taifa zima, kuhakikisha kila raia anapata nafasi sawa ya kushiriki uchaguzi huu, huku akiishi na akihisi amani na uadilifu vimewekwa mbele,” wameeleza.

Pia, wameeleza kuwa, wagombea wote wawe na nia safi ya kujenga amani na ustawi wa nchi, kwa kuwa kiongozi anayestahili kuingia madarakani ni yule anayeonesha uwajibikaji mbele ya Taifa.

Wamesisitiza ushindani kwa sera, lugha za kistaarabu, kuepuka upotoshaji na viongozi wazingatie maadili ili kujenga ustawi na kuimarisha amani na mshikamano zaidi.

Mchambuzi wa siasa, Said Majjid amesema waraka huo umebeba ujumbe mzito unaolenga makundi yote, wagombea, wananchi na mamlaka.

“Amani ni muhimu, ndani yake lazima tuzingatie haki, na ili haki ipatikane lazima kundi fulani liwajibike kwa nafasi yake. Ni waraka mzuri na unapaswa kuzingatiwa na kila mlengwa,” ameeleza.

Mchambuzi wa siasa, Mallya Manyinyi amesema amani ndio msingi wa kila kitu katika Taifa na hata familia.

Hata hivyo, amesema amani ina misingi yake ambayo ni haki, usawa na kuhakikisha kila mtu anapata kile anachostahili, hivyo makundi yote yazingatie hayo.