Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, ameahidi kuwa iwapo atarejea madarakani kwa muhula wa pili, Serikali yake itatoa kipaumbele kwa vijana na wanawake katika ajira.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, alipokutana na jumuiya za chama hicho katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
“Serikali nitakayoiunda nitajaza vijana na wanawake. Nikianza kutoa ajira, vijana wa hamasa wa CCM watakuwa kipaumbele,” amesema Dk Mwinyi, huku akikatishwa mara kwa mara na shangwe na vigelegele vya wanachama waliokuwa ukumbini.
Amesema kwa uwazi kuwa changamoto iliyopo ni vijana wanaotafuta ajira kushindwa kunufaika ipasavyo na nafasi zinazotolewa, jambo aliloliahidi kulishughulikia kwa kushirikisha Jumuiya ya Vijana ya chama na wadau wengine.
Amesema lengo ni kuhakikisha majina ya vijana wa CCM yanazingatiwa.
“Kama kuna jambo sipendi kulisikia ni kushindwa. Mnakumbuka mwaka 2020 tuliahidi ajira 300,000, lakini tumefanikisha ajira 217,000 sawa na asilimia 72. Tukirudi madarakani tunataka kuvuka lengo hilo na tayari mipango ipo,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema ajira zitapatikana katika sekta za Serikali ikiwamo elimu, afya na vikosi vya SMZ, pamoja na sekta binafsi kupitia uwekezaji wa viwanda vipya vinavyotarajiwa kujengwa.
“Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta mbalimbali, sasa nguvu zote zinaelekezwa kwenye ajira,” amesema mgombea huyo.
Awali, mwakilishi wa vijana, Zainab Mussa, aliwataka vijana kujitokeza kumpigia kura Dk Mwinyi, akisema ameonesha dhamira ya dhati ya kusaidia vijana kupata ajira na kujikwamua kimaisha.