FIFA yairuhusu Fountain Gate kusajili nje ya dirisha la usajili

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeridhia klabu ya Fountain Gate kufanya usajili nje ya dirisha la usajili

Hapo awali timu hiyo haikuruhusiwa kusajili kwani FIFA na TFF ziliifungia klabu hiyo kusajili kutokana na madeni waliyokuwa nayo na kuitaka kuwalipa wachezaji, na hata ilivyomaliza madeni bado mfumo wa usajili wa timu hiyo haukuwa umefunguliwa.

Katika taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema FIFA imeirufusu Fountain kusajili nje ya dirisha kutokana na sababu za kiufundi zilizojitokeza hadi timu hiyo kushindwa kufanya usajili kwa wakati.

“Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeridhia klabu ya Fountain Gate kufanya usajili nje ya dirisha la usajili kutokana na sababu za kiufundi”.

“Fountain Gate ilifungiwa na FIFA pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusajili kutokana na kudaiwa na waliokuwa wachezaji wake wawili wa kigeni. Ili iondolewe adhabu ya kufungiwa, Fountain Gate ilitakiwa kwanza iwe imewalipa wachezaji hao”.

“Klabu hiyo ilikamilisha malipo ya mchezaji wa mwisho tarehe 1 Septemba 2025, na siku hiyo hiyo FIFA iliondoa adhabu hiyo kwa barua”.

“Baada ya kufungiwa kwenye mfumo, Fountain Gate haikuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wapya isipokuwa kuhuisha (renew) wale waliokuwa wanaendelea nao kutoka msimu uliopita”.

“Licha ya kutuma barua hiyo, lakini FIFA haikuwa imefungua (unlock) akaunti ya usajili ya Fountain Gate hadi dirisha la usajili lilipofungwa tarehe 7 Septemba 2025, hivyo kuifanya klabu hiyo kushindwa kusajili wachezaji wapya”.

“Kutokana na hali hiyo, TFF ililazimika kuiandikia FIFA kuiomba iruhusu klabu hiyo iingize wachezaji wake kwenye mfumo kwa vile changamoto ilikuwa upande wake”.

“Baada ya FIFA kuridhia ombi hilo, na kwa kuzingatia kifungu cha 65(14) cha Kanuni za Ligi Kuu, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilikutana kwa dharura tarehe 6 Oktoba 2025 ambapo ilipitisha usajili wa wachezaji wapya wa klabu hiyo”.