Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, imetenga zaidi ya Sh 900 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mtambo mkubwa wa kisasa wa kuchonga miundombinu ya barabara korofi maeneo ya pembezoni.
Hatua hiyo imetajwa itakuwa mwarobaini kwa wakulima kuepuka walanguzi na kusafirisha wenyewe mazao kutoka mashambani kuingiza kwenye masoko na kuuza kwa bei nzuri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond Mweli ameliambia Mwananchi Digital leo Jumanne Oktoba 7, 2025 wakati akizungumzia mikakati ya kuongeza tija ya uzalishaji sambamba mwarobaini wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Kwa Wilaya ya Mbarali asilimia 80 ya mapato tunategemea zao la mpunga ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita zaidi ya Sh3.5 bilioni zilikusanywa na kuelekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hususani kuboresha miundombinu ya hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati katika Kata zote 20,”amesema.
Mweli amesema kutokana na mchango wa sekta ya kilimo, halmashauri kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga zaidi ya Sh 84.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa skimu 100 za umwagiliaji kwenye maeneo yenye changamoto ya maji.
“Lengo ni kuwaondoa wakulima na dhana ya kutegemea msimu wa mvua pekee ambayo wakati mwingine husababisha athari kutokana na uchache wake kutokidhi mahitaji ya mpunga unaozalishwa,” amasema Mweli.
Amesema mbali na programu ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji, halmashauri imeweka mikakati ya pamoja ya kuwakutanisha maofisa kilimo na wakulima kuzungumzia changamoto zinazo wakabilia katika uzalishaji na kuzitafutia majawabu.
Katika hatua nyingine Mweli, ametoa maelekezo kwa maofisa kilimo kuanza mara moja kuwaingiza kwenye mfumo rasmi wakulima ili waweze kutambulika, pia kuandika kwenye mbao za matangazo bei elekezi za pembejeo za kilimo.
Mkulima wa zao la mpunga Kata ya Rujewa wilayani humo, Steve Daniel amesema kitendo cha Serikali kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na barabara kutasaidia wakulima kurejesha matumaini ya kuongeza tija katika kilimo hicho.
Amesema changamoto kubwa kwenye uzalishaji wa zao la mpunga ni hali ya upatikanaji wa maji na ubovu muundo ya barabara jambo ambalo lilikuwa ni kilio kikubwa ambacho Serikali imesikia na kukifanyia kazi.