NSSF ARUSHA YAZINDUA MAADHIMISHO YA WIKI KWA WATEJA.

Na, Veronica Ignatus Michuzi Blog, Arusha. 

Mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii NSSF Jijini Arusha umefungua  maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, lengo likiwa ni kutoa shukrani kwa wananchama, motisha, kubainisha mafanikio pia changamoto za mfuko. 

Akifungua maadhimisho hayo Mkurugenzi mkuu wa Mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii (NSSF) nchini Masha Mshomba amesema huduma bora kwa wateja ni suala litakaloendelea kupewa kipaumbele kuhakikisha wanafikia lengo la mfuko. 

Aidha amesisitiza suala la ushirikiano wa kina kutoka kwa wadau ambao ni wafanyakazi na wateja wao. Amesema wateja wategemee kuona maboresho makubwa katika matumizi ya TEHAMA. 

“Tumefikia asilimia 97 kwa matumizi ya kidigitali, na tutahakikisha huduma zetu zinafika kila kona nchi nzima na kwa haraka, Juni 2025 tumefanikiwa kufikia mapato ya Trilioni 9.9, kwetu ni mafanikio makubwa tunawashukuru sana, bila nyinyi tusingefikia hatua hii kubwa”, 

“Tumefikia hayo kutokana na ushirikiano wetu wa dhati, kutoka kwa wadhamini wetu, Ofisi wa Waziri Mkuu na Benki Kuu, tunatamani ifikapo mwakani mfuko wetu ukue kufikia Tilioni 11.7” amesema Mshomba. 

Ametaja mafanikio makubwa ya mfuko kuwa ni wameweza kuwafikia wateja waliojiajiri ambao ndio wengi kwa takwimu nchini  na duniani kote kujiunga na mfuko. Amebainisha kuwa wataweza kupata mafao ya uzeeni, mafao ya uzazi kwa wanaojifungua, matibabu na huduma nyingine nyingi katika maisha. 

Hata hivyo katika kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za matumizi ya nishati safi kwa kila mtu ifikapo 2030, ambapo majiko takriban 100 yametolewa kwa waeja wakiwemo wastaafu. 

Kwa upande wake Meneja NSSF mkoa wa Arusha Josephath Komba ametoa shukrani zake kwa wadau wote kujumuika nao katika siku hiyo muhimu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, yaliyojumuisha waajiri, wafanyakazi wa mfuko, wananchama wanaojichangia kwa hiari na wastaafu. 

“Kipekee nawapongeza wafanyakazi wetu wa mfuko kwa kuchagua kaulimbiu ya ” Kidigitali Tumeweza” iliyosaidia kurahisisha utekelezaji wa majukumu, sambamba na hayo tumefanikiwa waajiri wetu kulipa michango ya wanachama kupitia lango la NSSF linalofahanika kama “Lango Portal” na kwa asilimia miamoja wote wanalipa kwa njia hiyo” amesema. 

Vile vile ametaja changamoto kadhaa ambazo ni baadhi ya Waajiri kuchelewa kuwasilisha michango ya wananchama,  hatua inayolazimu kuwatembelea na kufanya mazungumzo kwa lengo la kulinda wananchama. 

Katika namna hiyo Robert Kadeghe meneja huduma kwa wateja NSSF amesema maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka lengo likiwa ni kukutana na kutoa shukrani kwa wateja, kutoa tathmini ya mwenendo wa mfuko, kutambua mchango wa wanachama, kutambua wale waliofanya vizuri na kuwakumbusha wafanyakaz wa mfuko kutoa huduma bora.

Kadeghe amesema mfuko umewakumbuka wastaafu kuwa wanaweza kujihakiki kidijitali popote walipo pasipo kufika ofisi za NSSF, pia kupata maoni jinsi ya kuboresha huduma. 

Pia ameitaja “Kampeni ya Staa wa Mchezo Paka Rangi” inayolenga kuhamasisha waliojiajiri kuendelea kujiunga na mfuko huo, kwa kuwasilisha michango kila wakati. Kampeni hiyo ina umuhimu wa kipekee kwa wachangiaji wa hiari. 

“Tumedhamilia kutoa huduma bora kwa wateja, tumejipanga kuhakikisha tunamaliza kero zinazowakumba  wateja wetu” amefafanua.

Mmoja wa wateja wa NSSF Martin Mollel amepongeza huduma bora zinazotolewa na mfumo wa NSSF, ikiwemo bima za afya. 

“Maombi yangu kwenu, naomba watoto wasitolewe katika mpango wa bima ya afya anapofikisha umri wa miaka 18, bali atakapofikisha miaka 22 maana naamini atakuwa ameweza kujitegemea mwenyewe, pia kwa upande wa wananfunzi wanaosoma nje ya Arusha kuwekwe utaratibu watibiwe hukohuko mikoani maana naamini NSSF iko kila mahali” ameeleza Mollel.