Mgombea ubunge CUF auawa, wanane washikiliwa wakituhumiwa kuhusika

Siha. Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha, kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Kilimanjaro, Daudi Ntuyehabi  ameuawa na wananchi baada ya kudaiwa kumchoma mwenzake  kisu, Abdul Mohamed wakati akiamua ugomvi wa mgombea ubunge huyo na kijana mwingine ambaye waliyekuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ inayouza vinywaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea jana usiku, Oktoba 7, 2025  katika Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha.

Kufuatia tukio hilo, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mgombea ubunge huyo na kumsababishia kifo.

Kamanda Maigwa amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni, Hamadi Issah Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paulo Lutindi, Shedrack Emanuel, Jeremia Mnkondo, Zainab Elisha na Issah Mohamed.

Aidha, Kamanda Maigwa amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kuuawa kwa mgombea ubunge huyo.

“Mauaji hayo yametokea Oktoba 7, saa 1:30 usiku katika Kijiji cha Kilingi Sanya Juu, baada ya mgombea ubunge huyo  (marehemu) kumchoma kwa kisu tumboni na kusababisha utumbo kutoka nje Abdul Issah Mohamed, Mkazi wa Kilingi,” amesema.

Amesema, “Mohamed bado anaendelea na matibabu hospitalini na inadaiwa sababu za kuchomwa kisu ni kitendo chake cha kwenda kuamua ugomvi uliozuka kati ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) na Hamadi Issa Mohamed wakati wana kunywa pombe kwenye ‘grocery’ kutokana na kudaiana fedha.”

Aidha, Kamanda Maigwa amekemea tabia ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi kwani mara nyingi imekuwa ikisababisha madhara makubwa katika jamii.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kutoa wito na kukemea tabia ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi kwani mara nyingi imekuwa ikisababisha madhara makubwa kama haya yaliyotokea katika tukio hili,” amesema Kamanda Maigwa.