Watu 24 wauawa kwenye shambulio la kigaidi Myanmar

Myanmar. Watu zaidi ya 24 wameuawa na wengine 47 kujeruhiwa baada ya shambulio la kigaidi lililotokea katika tamasha na maandamano katikati mwa Myanmar.

Kwa mujibu wa msemaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (NUG) iliyo uhamishoni amesema tukio hilo lilitokea Jumatatu jioni katika Kitongoji cha Chaung U, wakati takribani watu 100 walipokuwa wamekusanyika kusherehekea Thadingyut, ambayo ni sikukuu ya kitaifa ya Wabudha inayoadhimisha mwisho wa Kipindi cha Kwaresima ya Kibudha.

Kwa mujibu wa  maofisa wa eneo hilo chini ya Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi (PDF) nchini humo kinachopambana na utawala wa kijeshi, parachuti yenye injini ilirushwa angani na kudondosha mabomu mawili kati ya umati wa watu waliokuwa wakishiriki tamasha hilo.

Tamasha hilo pia lilikuwa sehemu ya mkesha wa mishumaa kupinga sera za kijeshi linalotawala tangu mapinduzi ya mwaka 2021.

Mmoja wa maofisa wa PDF ameiambia BBC Burma kuwa walipokea taarifa za kijasusi kuhusu uwezekano wa shambulio la angani na walijaribu kusitisha mkusanyiko huo mapema, lakini waandamanaji walifika eneo la tukio kabla ya tahadhari hiyo kutolewa.

“Walifika na kurusha bomu ndani ya dakika saba tu,” amesema afisa huyo na kuongeza:

“Bomu la kwanza lilipoanguka, nilianguka chini na kugongwa goti, lakini watu waliokuwa karibu nami walikufa papo hapo,” amesema.

Myanmar imeendelea kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu jeshi lilipochukua madaraka Februari 2021, likimuondoa madarakani kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia, Aung San Suu Kyi. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa hadi sasa, mgogoro huo umesababisha mauaji ya raia takriban 5,000 nchini humo.