Msumi bado wasota kusaka maji

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi wakisotea huduma ya maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imeeleza kilichofanyika na jitihada zinazoendelea kutatua changamoto hiyo.

Dawasa imekiri kuwa huduma ya maji iliyopo kwa sasa haitoshelezi, hivyo kimetafutwa chanzo kingine ili kutatua kero hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, baadhi ya wakazi wa mtaa huo wameeleza changamoto wanayopitia ya kutafuta maji.

Godwin Mathias, anasema amefungiwa bomba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, lakini mara ya mwisho alipata maji Aprili, 2025 wakati wa masika, nayo aliyapata mara moja au mbili kwa wiki.

“Upatikanaji wa maji Msumi bado ni mbaya, licha ya viongozi kutupa matumaini kwamba kuna mradi wa Mbopo unakuja kutusuaidia,” amesema.

Naye, Beatrice Mwankire, mkazi wa eneo hilo amesema waliambiwa wasubiri kukamilika ujenzi wa miundombinu ya barabara ndipo watapelekewa mabomba na kwamba, hata maji ya chumvi waliyopata kutoka kwa wenye visima, sasa hawapati kwa sababu mabomba yamekatwa kutokana na ujenzi wa barabara unaoendelea.

“Licha ya kuwa tulikuwa tunauziwa uniti moja Sh5, 000 tofauti na bei ya Dawasa ya Sh1,700, bado yalikuwa mkombozi kwetu, hivyo kukatwa kwa mabomba kunazidi kutuumiza,” amesema.

Beatrice amesema maji ya Dawasa wanayopelekewa kwenye boza nayo yamepanda bei kutoka Sh15,000 hadi Sh20,000, huku upatikanaji wake ukiwa mgumu, kwani unaweza kukaa wiki ndipo unapelekewa tangu ulipoagiza.

“Maji yametufanya hata gharama za maisha kupanda, mimi mwenye familia kwa siku nanunua madumu yasiyopungua manane, kila moja ni Sh500, kwa kipato gani nilichonacho,” anahoji.

Amesema waliahidiwa wangepelekewa tanki maeneo yao, hivyo wangenunua maji Sh100 kwa ndoo, lakini mpaka leo Dawasa hawajapeleka.

Kwa upande wake, Salama Samata amesema kwa miezi mitatu maji ya Dawasa waliyoyategemea kutoka kwa majirani hawapati, jambo linalowafanya watumie ya chumvi.

Maria Ng’oja, ambaye tenki la maji ya Dawasa limewekwa nyumbani kwake, anasema huuza ndoo moja kwa Sh100. Hata hivyo, anasema wana miezi minne hawajapelekewa maji na hajui shida ni nini.

“Uhitaji wa maji eneo la Msumi Centre ni mkubwa, hatujui kwa nini siku hizi Dawasa hawatuletei maji licha ya kuwa tunawakusanyia hela yao. Tunahitaji maji kwani hayana faida kwa wanaokuja kuchota tu, bali hata sisi tulioachiwa jukumu la kuyauza pia tunafaidika nayo, kwa kuwa yakiisha hukosi Sh10, 000 hadi Sh15,000 na bado tunapata ya kutumia,” amesema.

Kwa mujibu wa Maria, tanki lililowekwa lina ujazo wa lita 10,000 na kila linapoisha wanapaswa kuwapatia Dawasa Sh35, 000 na  inayozidi ni mali yao.

Ally Kondo, anayeishi eneo la Kwa Panya, ambako kuna tanki la Dawasa, amesema kwa wiki hupelekewa maji mara moja na kutokana na uhitaji mkubwa, huisha ndani ya siku moja. Ameomba yapelekwe kila siku na matanki yaongezwe wakati wakisubiria kusambaziwa mabomba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msumi, Jackline Msafiri amesema kuna baadhi ya wanaouza maji hawapeleki fedha Dawasa.

“Baadhi ya wauzaji wamekuwa wakiingia tamaa ya hela wanazopata baada ya kuuza maji, wanazila, hivyo kusababisha wananchi wasipate huduma ya maji,” amesema.

Hata hivyo, amesema kuna mradi wameahidiwa utakaotatua changamoto ya upatikanaji wa maji, akitaka watafutwe Dawasa kuzungumzia suala hilo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro amesema ujenzi wa barabara ya Msumi kwenda Madale umesababisha kusimama kazi ya utandazaji wa mabomba, akisema kujengwa kwa barabara kuna faida nyingi kwao katika kukamilisha kazi hiyo.

Lyaro amesema kuna baadhi ya maeneo yanasubiri kukamilika ujenzi wa mabomba yanayokatiza barabara ili kuruhusu kupitisha miundombinu ya maji, kazi inayotekelezwa na mkandarasi wa barabara. Ameyataja maeneo hayo kuwa ni kuanzia Kanisa Katoliki hadi Kwa Mtenda.

Akijibu kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji katika Mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 walipanga kutekeleza miradi mitatu ya visima virefu, ambavyo vingechimbwa Msumi Shule ya Msingi, Msumi Zahanati na Msumi C.

Amesema hadi mwishoni mwa Julai, 2024 vilikuwa vimechimbwa kisima cha Shule ya Msingi Msumi kikiwa na uwezo wa kuzalisha  lita 6,000 kwa saa na kile cha Msumi Zahanati kikiwa na uwezo wa lita 4,000 kwa saa.

“Mradi wa kisima cha Msumi Shule ya Msingi umetekelezwa na kukamilika, lengo likiwa kuhudumia wanafunzi, walimu na wakazi jirani na shule. Kisima cha Msumi Zahanati kitaendelezwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kuhudumia zahanati na wakazi waliopo jirani,” amesema na kueleza kuwa, mradi wa kisima cha Msumi shule unanufaisha watu 2,882.

Hata hivyo, amesema maji ya visima hivyo hayatoshelezi mahitaji ya wakazi wa Mtaa wa Msumi, hivyo ilishauriwa kutafuta chanzo kingine kuwezesha kutekeleza mradi mkubwa utakaokidhi mahitaji, hivyo ilibainishwa kutumika tanki la maji la Tegeta A.

“Usanifu umefanyika na utekelezaji wa mradi huu umeanza Aprili 16, 2025. Mradi wa maji Msumi kwa kutumia tanki la Tegeta A unaenda kunufaisha wakazi wa Mtaa wa Msumi, likiwamo eneo la Msumi C na baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Tegeta A,” amesema.  

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha watu 47,862 kutoka Mtaa wa Msumi (Msumi A, B na C) pamoja na wakazi wa mtaa wa Tegeta A.

“Mtaa wa Msumi unahitaji kubwa la huduma ya majisafi na salama. Kukamilika kwa mradi wa maji Msumi kutumia kisima cha Msumi Shule ya Msingi na tanki la Tegeta A kunaenda kuwa suluhisho la kero ya maji kwa wakazi wa Mtaa wa Msumi na Mtaa wa Tegeta A. Jumla ya watu 50,744 watahudumiwa,” amesema.