INEC yasitisha kampeni kifo cha mgombea ubunge wa CUF Siha

Moshi. Kutokana na kifo cha aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Daudi Ntuyehabi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesitisha shughuli za kampeni za ubunge katika jimbo hilo hadi maelekezo mengine yatakapotolewa.

Ntuyehabi, alifariki dunia Oktoba 7, 2025  baada ya kushambuliwa na kundi la watu zaidi ya wanane wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja wakati alipokwenda kuamua ugomvi wa mgombea huyo na mtu mwingine ambaye walikuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ ya vinjwaji.

Katika tukio hilo, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mgombea ubunge huyo na kumsababishia kifo chake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Msimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jimboni humo, Marco Masue amesema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi mgombea ubunge anapofariki na ikathibitishwa na INEC shughuli za kampeni za ubunge katika jimbo hilo zinasitishwa mpaka itakapotangazwa vinginevyo.

Aidha, amesema shughuli za kampeni za urais na madiwani katika Jimbo hili zinaendelea kama kawaida.

Akitoa pole kwa familia ya mgombea huyo, Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Siha, Adam Ramadhan amesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mgombea huyo