Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jukwaa la Watendaji Wakuu (CEO Roundtable of Tanzania – CEOrt) katika kuimarisha majadiliano yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha utekelezaji wa sheria za kodi kupitia sekta binafsi, ili kuongeza mapato kwa maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo, Jumatano Oktoba 8, 2025, katika kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na CEOrt, ambacho kimewakutanisha viongozi waandamizi wa TRA, wanachama wa CEOrt, wataalamu wa masuala ya kodi na wawakilishi wa Serikali.
Mjadala huo umelenga kuimarisha usimamizi wa kodi, kuongeza ushirikiano na kubaini maeneo ya kipaumbele ya marekebisho ya sera kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi.
Akihutubia kikao hicho, mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema taasisi hiyo kwa sasa inabadilisha mwelekeo wake kutoka kutumia nguvu hadi kujenga mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
“Mwelekeo wetu sasa ni kuwezesha badala ya kulazimisha. Mfumo wa kisasa wa kodi unatakiwa kuirahisishia biashara kutekeleza wajibu wake, kukua na kuajiri.
“Tunapolenga Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ushirikiano na sekta binafsi kupitia CEOrt ni msingi wa kujenga uchumi jumuishi na imara,” amesema Mwenda.
Aidha, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwamo kuanzisha Kamati ya Kitaifa ya Mapitio ya Kodi, ambayo baadhi ya wajumbe wake ni wanachama wa CEOrt.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya CEOrt, David Nchimbi, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kodi iliyo wazi na inayotabirika, akieleza kuwa hilo linaongeza imani ya wawekezaji na kuharakisha maendeleo endelevu.
“Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa mazungumzo ya wazi kati ya Serikali na sekta binafsi, jambo linalosaidia kufanikisha marekebisho ya sera zinazokubaliana na uhalisia wa biashara,” amesema Nchimbi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CEOrt, David Tarimo, amesema majadiliano hayo yamejikita katika maeneo muhimu ikiwamo makadirio ya kodi, urahisishaji wa uzingatiaji wa sheria na kujenga imani kati ya TRA na jamii ya wafanyabiashara.
“CEOrt itaendelea kuwa kiunganishi muhimu katika majadiliano yenye ushahidi kati ya sekta binafsi na Serikali. Mazungumzo ya dhati na yenye kuheshimiana yanawezesha kupatikana suluhisho linaloimarisha ufanisi wa utawala na ustawi wa biashara,” amesema Tarimo.
Washiriki wa mkutano huo wamepongeza hatua ya TRA kuendeleza mageuzi ya kidijitali, huku wakisisitiza haja ya tafsiri ya sheria za kodi kufanywa kwa usawa katika sekta zote.
Kikao hicho kimefanyika wakati ambapo TRA imeripoti mafanikio ya makusanyo ya mapato. Katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, mapato ya ndani yamefikia Sh8.97 trilioni, yakizidi lengo kwa zaidi ya asilimia 6, hatua inayodhihirisha ufanisi wa mageuzi yanayoendelea.
CEOrt, ambayo inajumuisha zaidi ya taasisi na kampuni 230 kutoka sekta mbalimbali, mwaka huu inasherehekea miaka 25 ya kuendeleza sekta binafsi nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jackline Woiso, ambaye pia ni mwanachama wa CEOrt, amesema ana matumaini makubwa kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali katika kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji na ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.