Shauri la kutekwa  Polepole kuanza kesho  mahakamani

Dar es Salaam.  Shauri la kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, limeitwa mahakamani kesho, kwa ajili ya usikilizwaji kwa hatua ya awali.

‎‎Shauri hilo la maombi ya amri ya kufikishwa mahakamani kwa lugha ya kisheria ‘Harbeas Corpus’ limefunguliwa na mawakili wa Polepole, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba yake Polepole.

‎‎Katika shauri hilo wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP),  Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZPC).

‎‎Kwa mujibu wa hati ya wito wa Mahakama kwa pande zote ambayo Mwananchi imeiona na kuthibitishwa na Wakili Kibatala, leo Jumatano, Oktoba 8,2025, limepangwa kusikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Salma Maghimbi.

‎‎Kwa mujibu wa wito huo, shauri hilo limeitwa mbele ya Jaji Maghimbi kesho Alhamisi, Oktoba 9, 2025 saa 3:00 Asubuhi.

‎‎”Shauri limeitwa mbele ya Jaji Maghimbi kesho tarehe 9, 2025, kwa ajili ya maelekezo. ‘Summons’ (hati za wito wa Mahakama) zimeshatolewa kwa wahusika wa pande zote katika shauri tajwa”, amesema Wakili Kibatala.

‎‎Shauri hilo lilifunguliwa mahakamani hapo jana Oktoba 7, 2025, chini ya hati ya dharura.

‎‎Katika  hati hiyo ya dharura iliyothibitishwa na Wakili Kibatala, inaeleza kuwa, tangu juzi Oktoba 6, 2025, Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi  waliovamia nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

‎‎Pia, wakili Kibatala anadai kuwa mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika Mahakama yoyote ya kisheria na kwamba inaaminika kuwa amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.

‎‎”Hivyo haki zake za Kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi,” amesema Kibatala.

‎‎”Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwamo kujua hali ya maisha yake.”

‎‎Katika hati maombi, wanaomba wasikilizwe upande mmoja na Mahakama iamuru Polepole afikishwe mahakamani wakati akisubiri uamuzi wa maombi hayo kusikilizwa pande zote.

‎‎Katika usikilizwaji wa maombi hayo, pande zote wanaomba Mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamuachilie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika Mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.

‎‎Maombi hayo yanaungwa mkono na kiapo kilichoapwa na Wakili Kibatala.

‎‎Katika kiapo hicho, Wakili Kibatala anaeleza kuwa, mwombaji, Polepole ni raia wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi yake katika nafasi mbalimbali ikiwamo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Cuba na nchi nyingine za Kilatini.

‎‎Pia, anaeleza kuwa katikati ya mwaka huu, Polepole kwa hiyari yake alijiuzulu wadhifa huo wa ubalozi huki alieleza sababu mbalimbali zikiwamo kutokuridhika na namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya Serikali.

‎‎Wakili Kibatala anaeleza kuwa, katika taarifa zake ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara, Polepole amekuwa akilalamikia usalama wake uko hatarini kutokana na vitisho ambavyo amekuwa akivipokea kutoka kwa watu wasiojulikana kutokana na msimamo wake katika masuala mbalimbali.

‎‎Hivyo, anadai kuwa wakati fulani alfajiri ya Oktoba 6, 2025, wavamizi wasiojulikana waliovamia na kuvunja katika makazi yake ya muda, Ununio jijini Dar es Salaam na walimteka kumpeleka mahali kusikojulikana.

‎”Haya yamethibitishwa kwa umma na kaka wa mwombaji (Polepole), Godfrey na Augustino Polepole, kama ilivyothibitishwa katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani,” amesema Wakili Kibatala katika kiapo hicho.

‎‎Wakili Kibatala anaeleza kuwa, kuwa mjibu maombi wa tano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Jumanne Muliro amenukiliwa katika taarifa hizo za vyombo vya habari akitoa taarifa za kupuuza tuhuma hizo nzito za utekwaji wake.

‎‎Amesisitiza kuwa mpaka wakati anaapa kiapo hicho, mwombaji Polepole hajulikani mahali alipo na hakuna hata mmoja kati ya wajibu maombi ambaye ametoa mrejesho wowote kuhusu alipo, hali yake ya ustawi na hadhi yake ya kisheria; jambo linaloongeza kiwango cha wasiwasi nchini.

‎‎”Nina sababu za kuamini kwamba wajibu maombi na hasa mjibu maombi wa tano, ZPC ana ufahamu na yuko na mamlaka ya kumshikilia mwombaji,” amesema Wakili Kibatala. 

‎‎Polepole aliyetangaza kujiuzulu wadhifa wa ubalozi huo kwa kuiandikia barua ya kujiuzulu kwake mamlaka ya uteuzi wake; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julai 13, 2025, usiku wa kuamkia Oktoba 6, 2025 alichukuliwa na watu wasiojulikana.

‎‎Taarifa za kutekwa kwake zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana Oktoba 6, 2025, kupitia picha jongefu (video clip) iliyorushwa mitandaoni ikimuonesha mtu aliyejitambulisha kwa jina la Augustino Polepole.

Katika video hiyo, Augustino ambaye alijitambulisha kuwa ni kaka wa Humphrey, alieleza kuwa Polepole alichukuliwa na watu waliovamia nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.