Bashiru: Anayesema vijana watavunja nchi siwaelewi

Mwanza. Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ali, ameeleza kuwa kutokana na uwezo wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Samia Suluhu Hassan wa kuhimili changamoto mbalimbali zilizoitikisa nchi, Tanzania itabaki salama na hawaelewi watu wanaosema vijana watavunja nchi yao.

Aidha amewahakikishia Watanzania kuwa mgombea huyo wa CCM, ni kiongozi ambaye ameshakutana na majaribu mengi na ameweza kuyashinda.

Amesema mambo yanayoweza kutoa Taifa kwenye mstari wa kulijenga   hayapaswi kuendekezwa na wala majaribio ya kutikisa misingi na amani ya nchi yasipuuzwe.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 8, 2025 katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza, kwenye kampeni za mgombea urais wa chama hicho.

“Mtu anayesema vijana watavunja nchi simwelewi, vijana wa Tanzania hawawezi kuvunja nchi yao,” amesema.

Akizungumzia uwezo wa mgombea urais, Bashiru amewahakikishia Watanzania kuwa mgombea huyo ni kiongozi ambaye ameshakutana na majaribu na ameshinda.

“Nasikia maneno kuhusu uwezo wa mgombea wetu, niwahakikishie huyu ni kiongozi ambaye anaomba ridhaa na ameshakutana na majaribu, ameshajaribiwa na ameshinda majaribu tuna uhakika tutavuka salama,”

“Kama nchi yetu imebaki moja, CCM imeendelea kuwa moja, usalama na amani imetamalaki tena katika kipindi kigumu cha mabadiliko ya Serikali ya ghafla (baada ya kufariki Rais wa awamu ya tano, hayati  John Magufuli).”

“Hivi vimaneno maneno kuna watu wamepanga. Simaanishi tupuuze majaribio ya kutikisa amani ya nchi yetu au jaribio la kutikisa misingi na amani ya nchi yetu…

“Huyu kiongozi ni hazina ya uzoefu wa kiongozi katika vipindi vigumu na mimi sina mashaka na Watanzania waliompa ushirikiano ndio haohao waliomuombea dua na wanaoendelea kumuombea kura. Watanzania wanaotangaza kazi njema ni hao ambao anawaongoza, tusipuuze lakini tusiendekeze mambo ambayo yanaweza kututoa kwenye mstari wa kujenga Taifa letu,” ameongeza.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda amewataka Watanzania wakiwemo vijana kumlinda mgombea urais huyo.
Kwa upande wake waziri wa zamani wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu ameelezea mafanikio ya sekta ya afya aliyofanya Samia katika kipindi cha miaka minne huku akitolea mfano ajali ya basi la wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Lucky Vincent, Mei 6,2017 eneo la Karatu na kusababisha vifo vya wanafunzi 32,walimu wawili na dereva mmoja huku wakinusurika wanafunzi watatu.

Amesema Samia akiwa Makamu wa Rais kipindi hicho alifika kuongoza kuaga waliofariki na kuwa alielekeza majeruhi hao kutibiwa popote ambao walienda kutibiwa nje ya nchi na kupona na sasa wanasoma Chuo Kikuu Marekani.

“Wakati watu zaidi ya laki moja uliwatazama watoto waliokuwa wanaagwa ulitoa machozi ulitazama janga linaloikumba Tanzania ukajikuta unatoa machozi, ukajikita katika dhana ya utu na kuhakikisha Taifa linaboresha sekta ya afya,”

“Nakumbuka miaka minne umejenga hospitali za wilaya 129,vituo vya afya 1,300 na hospitali zenye uwezo wa kuhudumia dharura zimeongezeka hadi kufikia 113.Sasa hivi watu wanatoka nchi jirani kama Burundi, Malawi na Msumbiji wanakuja Tanzania kufanya utalii wa matibabu,”amesema.