Simulizi ya familia ya mgombea ubunge CUF aliyeuawa

Familia ya mgombea ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Jimbo la Siha, Daudi Ntuyehabi, ambaye amefariki baada ya kushambuliwa na kundi la watu zaidi ya wanane, imeeleza ilivyopokea taarifa za kuuawa kwa ndugu yao na kuiomba Serikali kuingilia kati na kuchukua hatua kwa waliohusika na mauaji hayo ya kikatili.

Akizungumza dada wa mgombea huyo, Annet Ntuyehabi amesema kifo hicho kimekatisha ndoto za ndugu yao aliyekuwa akitaka kuongoza wananachi wa jimbo hilo kupitia nafasi ya ubunge. Aidha, amesema kifo chake kimeacha pengo kwa familia kwa kuwa alikuwa ni baba wa watoto wawili, mmoja darasa la nne na mwingine darasa la kwanza.

Shemeji wa marehemu, Rogate Mwandry amesema kifo cha ndugu yao wameiachia Serikali na kwamba kimeacha pengo kubwa kwa familia. Akizungumzia kuhusu mazishi ya ndugu yao, shemeji wa marehemu, Alpha Mwandry, amesema kwa sasa wanasubiri baadhi ya ndugu kutoka Geita kwa ajili ya mipango ya mazishi. 

Ntuyehabi, alifariki dunia Oktoba 7, 2025  baada ya kudaiwa kushambuliwa na kundi la watu zaidi ya wanane wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja wakati alipokwenda kuamua ugomvi wa mgombea huyo na mtu mwingine ambaye walikuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ ya vinjwaji.

Katika tukio hilo, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mgombea ubunge huyo na kumsababishia kifo chake.