ACT Wazalendo yaja na Ilani ya wananchi Zanzibar

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT–Wazalendo na mgombea urais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema ilani ya uchaguzi ya chama hicho inalenga kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali kwa kusimamia masuala ya msingi yanayogusa maisha ya kila mmoja, ikiwamo elimu bora, afya, ajira zenye tija na hifadhi ya jamii.

Akizindua ilani hiyo leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 mjini Unguja, Othman amesema chama chake kimejikita katika kuandaa sera zinazojibu changamoto zinazojirudia kila mara visiwani humo, ikiwamo ukosefu wa ajira kwa vijana, huduma duni za afya na mfumo wa elimu unaoendelea kudorora.

“Kile ambacho Zanzibar inahitaji kwa sasa ni mageuzi makubwa ya kurejesha thamani ya utu na maisha ya kila mtu. ACT–Wazalendo imekuja na ilani inayojikita katika kusuluhisha changamoto hizo,” amesema Othman.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa chama hicho, akiwamo Makamu Mwenyekiti wa ACT–Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa, pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho.

Othman ameeleza kuwa sera za chama chake zimejikita kwenye misingi minne mikuu ya uchumi kupitia kilimo na uvuvi wa kisasa, utalii wa staha, ujasiriamali na viwanda vya kuongeza thamani, ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu mamlaka, amesema chama chake kinauchukulia Muungano kama eneo la haki na si fadhila, hivyo Zanzibar kama mshirika kamili inapaswa kuwa na mamlaka na heshima inayostahiki.

Akifafanua zaidi, amebainisha kuwa ACT–Wazalendo pia imeweka kipaumbele katika mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa, kurejesha utawala wa sheria na kulinda thamani ya fedha za umma.

Kwa upande wa sera za kijamii, Othman amesema chama chake kitaimarisha utengamano wa kijamii kupitia maridhiano ya kweli, mageuzi ya maadili na malezi ya watoto kwa kuzingatia silka za Kizanzibari.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, amesema mambo matano ya msingi yaliyowekwa katika ilani hiyo ni pamoja na mamlaka ya Zanzibar na utawala, mapitio ya mkataba wa Muungano na mabadiliko ya Katiba, utengamano wa kijamii na utamaduni, mageuzi ya mafunzo ya maadili na malezi ya watoto, pamoja na kuimarisha uchumi shirikishi.

Othman amesema ilani yao ya uchaguzi kwa upande wa Zanzibar inalenga kuleta mageuzi makubwa katika utawala, uchumi na jamii ifikapo mwaka 2030, ili kurejesha matumaini ya wananchi na kujenga mustakabali mpya wa visiwa hivyo.

Amesema kipaumbele kimewekwa kwenye mageuzi ya mifumo ya kisheria, uchaguzi na haki za binadamu, pamoja na kuimarisha uchumi shirikishi kupitia mageuzi ya kikodi, hifadhi ya jamii na sekta za kilimo na biashara.

“Na tano ni teknolojia na maendeleo endelevu, tutasimamia mageuzi katika huduma za habari, mawasiliano na utafiti kwa maendeleo,” amesema Othman, akiwataka wanahabari kuhakikisha ujumbe wa ilani hiyo unawafikia Wazanzibari.

Amesema huu ni wakati wa ACT–Wazalendo kuleta mabadiliko makubwa na si chama kingine, akisisitiza; “Wazanzibari, Oktoba 29 tusifanye kosa la kurudi kwenye giza la miongo iliyopita. Ni ACT–Wazalendo pekee inayoweza kufanya mabadiliko kwa sababu inaweza na inajiamini.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya ACT–Wazalendo (Zanzibar), Profesa Omar Fakih, akiwasilisha muhtasari wa ilani hiyo, amesema mwelekeo wake umetokana na maoni ya wananchi na kugusa moja kwa moja changamoto zinazowakabili.

Amesema ilani hiyo imejikita katika mambo kumi yanayowanyong’onyesha Wazanzibari, yakiwamo ukosefu wa ajira zenye tija, mifumo ya fedha na mikopo inayodumaza uchumi, biashara na viwanda visivyopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, changamoto za nishati na maji, uhalifu, ufisadi na kutokuwepo kwa utii wa sheria.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni matumizi mabaya ya taaluma, umasikini uliokithiri, kukosekana kwa usawa, kilimo kisicholeta tija, mfumo wa elimu ulioshindwa kuihudumia Serikali na jamii, pamoja na huduma za afya zilizoshindikana kusimamiwa ipasavyo.

Profesa Fakih amesema ifikapo mwaka 2030, ACT–Wazalendo inalenga kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mamlaka kamili ya kitaifa na kimataifa, ikisimamia uchumi wake kupitia rasilimali na sheria zake, huku ikiheshimu makubaliano ya Muungano yenye usawa na heshima.

“Kuhusu utengamano, tunataka kuona Zanzibar ifikapo mwaka 2030 ikijivunia mshikamano wa kijamii na utamaduni wa Kizanzibari unaojenga mshikamanisho na kusaidiana,” amesema.

Aidha, amesema chama hicho kinapanga kuibadilisha Zanzibar kuwa kitovu cha utalii wa hadhi ya kimataifa kwa kuzingatia miundombinu ya kisasa, usimamizi bora wa mazingira na sera za utalii rafiki wa mazingira.

Kwa upande wake, Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano wa ACT–Wazalendo, Salim Biman, amesema tukio hilo ni la kihistoria na limeweka wazi ramani ya jinsi Zanzibar itakavyoongozwa chini ya Othman Masoud kuanzia Oktoba mwaka huu.

“Hii ni ilani bora yenye mwelekeo na matumaini, ambayo Wazanzibari wataifurahia kwa sababu imegusa mustakabali wao,” amesema Biman.