WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yatazinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Aidha, amesema uzinduzi wa Maadhimisho hayo yatafanyika katika Viwanja vya Uhindini Jijini Mbeya.
Mhe. Ridhiwani amesema hayo leo tarehe 8 Oktoba, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa Habari, katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Waziri Ridhiwani Kikwete amesema Wiki hiyo huadhimishwa kila Mwaka Oktoba 8 hadi 14 kwa kuwakutanisha vijana kutoka Tanzania bara na Visiwa kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, kwa lengo la kujadiliana, kuonesha vipaji, bunifu na kazi wanazozifanya.
Vile vile, amesema shughuli zitakazofanyika kwenye wiki hiyo ni pamoja na kuwapo na makongamano ya kuwajengea uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri , elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.
Kwa upande mwengine, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema maadhimisho hayo ya Wiki ya Vijana yataambatana na maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika katika uwanja wa CCM-Sokoine Mkoani Mbeya tarehe 14 Oktoba, 2025.
Kwa upande mwengine, Waziri Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya na Mikoa jirani, kujitokeza kwa wingi katika eneo la maonesho ya wiki ya vijana na katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.