Lissu alivyomalizana na shahidi kesi ya uhaini

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu Leo amemaliza kumuuliza maswali shahidi wa kwanza wa Jamhuri kutokana na ushahidi wake alioutoa mahakamani hapo Oktoba 6 ,2025.

Hata hivyo Kesi hiyo imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 9 saa tatu asubuhi ambapo  itaendelea katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam kwa upande wa mashtaka kuendelea kumuhoji shahidi huyo wa kwanza maswali ya msawazisho, yenye lengo la  kufafanua mambo mbalimbali yaliyoibuka katika maswali aliyoulizwa na mshtakiwa.

Lissu amerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili halina dhamana, huku akitimiza  siku 183  tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025.

Kwa mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani iliyopelekwa kwa pande zote, kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Oktoba 6 mpaka Oktoba 24, 2025.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.