Taifa Stars, Zambia mechi ya heshima

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo Jumatano inahitimisha safari ya kutafuta nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kucheza na Zambia kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Stars ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi E ikiwa na pointi 10 nyuma ya Morocco yenye pointi 21 ambayo tayari imefuzu, inakabiliana na Zambia iliyopo nafasi ya nne ikiwa na pointi sita.

Katika mechi iliyopita baina ya timu hizo Stars ikiwa Zambia ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Wazir Junior, hivyo kuweka matumaini ya kufanya vizuri kwenye kinyang’anyiro hicho kabla ya mambo kugeuka na kudondosha pointi mbele ya Morocco, Congo na Niger.

Taifa Stars ilifungwa nyumbani na Morocco kwa mabao 2-0, ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Congo kabla ya kuchapwa 1-0 na Niger jambo ambalo limewafanya vijana wa kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ kushindwa kuwa na nafasi ya kucheza mchujo.

TAIFA 01

Pamoja na kwamba vinara wa makundi tisa wanafuzu moja kwa moja, timu nne ambazo hushindwa kumaliza vinara kwenye makundi zinapata nafasi ya kucheza mchujo unaoanzia nusu fainali kisha fainali na mshindi ataungana na wawakilishi kutoka mabara mengine.

Timu ambazo zinaonekana kuwa na nafasi kubwa kupenya kupitia mlango huo ni Gabon yenye pointi 19, Madagascar na DR Congo zote zina pointi 16 na Burkina Faso, Cameroon, Namibia na Uganda kila moja pointi 15, hivyo itategemea na mechi za mwisho.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Taifa Stars, Morocco alisema: “Haitakuwa mechi nyepesi hata kidogo kwa sababu Zambia ni miongoni mwa mataifa shidani, hivi karibuni wamekuwa wanapitia kipindi kigumu lakini hilo haliwezi kuondoa ubora wao. “Tumejiandaa vya kutosha na naamini tutafanya vizuri na kuwapa burudani mashabiki wetu.”

TAIFA 02

Kwa upande wa kiungo wa Zambia, Clatous Chama ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kwani anaamini mechi hiyo itakuwa nzuri na yenye ushindani.

“Tanzania ni wapinzani wagumu, tumekuwa tunafahamiana kwa hiyo itakuwa mechi nzuri,” alisema Chama.

Licha ya Taifa Stars kuichapa Zambia katika mechi ya mwisho ikiwa ugenini, rekodi inaonyesha kuwa Tanzania imekuwa ikishindwa kutamba ikiwa nyumbani dhidi ya timu hiyo. Katika mechi tano ikiwa za kirafiki imetoa sare mbili na kuchapwa tatu.