KUNA hesabu kubwa zinaendelea ndani ya Yanga, uongozi wa klabu hiyo umefikia ukingoni mwa mchakato wa kumpata kocha mpya, huku ikielezwa kwamba endapo watamalizana na Romain Folz basi Romuald Rakotondrabe “Roro” wa Madagascar ndiye atakayeshika usukani.
Kwa waliofuatilia michuano ya CHAN PAMOJA 2024, jina la Roro si geni. Yeye ndiye aliyoiweka Madagascar kwenye ramani ya soka la ndani Afrika baada ya kuipeleka hadi fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao, wakipoteza kwa Morocco kwa mabao 3–2.
Huo ulikuwa mwanzo wa zama mpya kwa taifa lililokuwa likihesabiwa kama “underdog”.
Lakini nini hasa kinamfanya Roro kuwa tofauti? Na je, falsafa zake za kiufundi zinaweza kuibadilisha Yanga na kuwa tishio Afrika kama ilivyokuwa kwa Madagascar katika mashindano ya CHAN ambayo yalifanyika kwa mara ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki? Katika uchambuzi huu, kuna ubora wake na udhaifu alionao.

NIDHAMU NA UMOJA
Ukiwa na timu iliyo na wachezaji wenye vipaji vikubwa kama Pacome Zouzoua, Prince Dube au Clement Mzize, changamoto kubwa ni kuhakikisha kila mmoja anacheza kwa nidhamu ndani ya mfumo. Hapa ndipo Roro anapoonekana kuwa chaguo sahihi zaidi kwa Yanga.
Kocha huyo anaamini kuwa ushindi unajengwa kwenye umoja na wala sio uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Alipokuwa Madagascar, alitengeneza utamaduni wa nidhamu ya kimbinu uliowafanya wachezaji wa ndani kuonekana kama nyota wa Ulaya. Kila mchezaji alifahamu wajibu wake, walijua muda wa kushambulia na kurudi nyuma kulinda matokeo.
Ikiwa Roro ataingia Yanga, basi nidhamu hiyo ndiyo itakayokuwa msingi wa mafanikio mapya ya klabu hiyo. Yanga ambayo mara nyingi imekuwa bora katika kushambulia, anaweza kuipa uwiano bora zaidi.

UWEZO WA KUBADILIKA
Roro ni kocha anayejulikana kwa kubadilisha mfumo kulingana na mpinzani. Wakati Madagascar ilipokutana na timu zinazocheza kwa presha ya juu kama Kenya au Burkina Faso, Roro alitumia muundo wa 4-1-4-1, lakini walipocheza dhidi ya wapinzani wanaocheza taratibu, alihamia kwenye 4-3-3.
Kwa Yanga, hii inaweza kuwa silaha hatari. Kwa mfano, dhidi ya Simba ambayo hupenda kushambulia kupitia pembeni na “wing overlaps”, Roro anaweza kuamua kutumia 3-5-2 yenye ukuta imara katikati huku akitumia ‘wing-backs’ wanaorudi kwa kasi Israel Mwenda na Chadrack Issaka Boka.
Lakini anapocheza na miamba zaidi ya soka la Afrika katika michuano ya kimataifa kama vile Mamelodi Sundowns na hata Al Ahly anaweza kubadilika haraka na kutumia ‘compact 4-4-2’ ili kudhibiti eneo la kati.
Kwa maneno mengine, Yanga ya Roro haitakuwa timu inayocheza kwa mfumo mmoja, itakuwa timu inayosoma wapinzani na kubadilika kwa haraka.

UELEWA WA WACHEZAJI
Roro si tu kocha wa mazoezi ya uwanjani ni mwanasaikolojia mzuri.
Alijenga kitu kinachoitwa “Barea Mentality” kwenye kikosi cha Madagascar kuamini kwamba ukubwa wa mpinzani haumaanishi kushindwa.
Hii ilijidhihirisha pale Madagascar ilipoitoa Sudan kwenye nusu fainali kwa ushindi wa 1-0 na kuonyesha utulivu mkubwa hata kwenye uwanja wenye mashabiki zaidi ya 50,000.
Kwa Yanga, hii ni falsafa itakayoongeza nguvu ya kiakili kwenye mechi kubwa za Afrika. Kikosi chao kina wachezaji wenye uzoefu lakini mara nyingine hukosa msukumo wa kisaikolojia wanapokutana na vigogo wa soka la Afrika, mechi ambazo huhitaji zaidi ya ubora wa timu uwanjani.
Roro anaweza kubadilisha hilo kwa kuwajenga kiakili kupitia misingi ya nidhamu na umoja.

SOKA LENYE UTAMBULISHO
Wakati Yanga ya Folz ikionekana kupata matokeo huku ikicheza soka ambalo linaonekana kutovutia kwa wengi, Roro anakuja na kitu tofauti, soka lenye uwiano wa kushambulia na kulinda.
Hana hofu ya kuachia mpira kwa wapinzani kama itahitajika, lakini anasisitiza kuwa kila pasi iwe na maana.
Madagascar chini yake ilicheza soka lililokuwa na ‘transition speed’ yani sekunde chache kutoka eneo la nyuma hadi kwa wapinzani. Wachezaji kama Mudathir Yahya na hata Aziz Andabwile watapata nafasi ya kucheza kwa uhuru zaidi katika kuanzisha mshambulizi eneo la kati wakitumia kasi ya Nzengeli na Zouzoua kupasua mipango ya wapinzani.
Roro anaamini katika mafunzo ya mbinu “tactical drills” kuliko mazoezi ya muda mrefu ya stamina. Hii inaweza kuifanya Yanga iwe timu yenye uelewa mkubwa wa nafasi, kitu ambacho kinahitajika katika michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

KUKUZA VIPAJI VYA NDANI
Roro amekuwa akihusishwa sana na falsafa ya wachezaji wa ndani “local empowerment”. Nchini kwake, alitoa nafasi kwa wachezaji wa ndani kuonyesha uwezo hata mbele ya wale wanaocheza Ulaya. Uamuzi huo uliibua nyota wapya na kuongeza ushindani wa ndani.
Kwa Yanga, hii inaweza kuwa nafasi ya kuona vijana kama Abdulnasir Abdallah ‘Casemiro, Shekhani Khamis au Denis Nkane wakipata nafasi ya kutumika zaidi katika michuano mikubwa.
Kwa mfumo wa Roro, kila mchezaji anapimwa kwa nidhamu na uwezo wa kiufundi na sio ukubwa wa jina lake.

UDHAIFU
Katika kila kitu chenye ubora, ndani ya kuna upungufu. Kwa Roro, timu yake licha ya kuwa nzuri katika kushambulia na kulinda, lakini ina changamoto kwenye ulinzi pindi inapokuwa kwenye wakati wa kusaka bao au kulinda ushindi.
Ukiangalia katika mashindano ya CHAN 2022 nchini Algeria wakati Madagascar ikimaliza nafasi ya tatu, timu hiyo iliruhusu mabao matatu pekee katika mechi tano, ikifunga mabao tisa.
Clean sheet mbili. Hapo kwa kiasi fulani alifanikiwa kulinda.
Katika CHAN 2024, Madagascar ilicheza mechi saba, ilifunga mabao tisa na kuruhusu saba ikiwa na cleansheet mbili pekee, huku timu hiyo ikimaliza nafasi ya pili ikipoteza mechi ya fainali dhidi ya Morocco kwa mabao 3-2.
Kufunga mabao tisa na kuruhusu saba, ni wazi kulikuwa na nidhamu mbovu kwenye ulinzi. Mechi ya fainali dhidi ya Morocco, Madagascar ilianza kufunga dakika ya 9, wapinzani wakasawazisha dakika ya 27. Ilipokuwa inasaka bao la kuongeza, ikajikuta ikiruhusu dakika ya 40 na kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
Dakika ya 68, ikasawazisha, sasa ikawa inafanya kazi ya kulinda angalau ipate sare ili mshindi aamuliwe kwa penalti. Kosa likafanyika na kuruhusu bao dakika ya 80, shughuli ikaishia hapo.