BAADA ya Mabaharia wa KMKM kupoteza mechi dhidi ya KVZ kwa kufungwa mabao 2-0 kisha kuambulia sare mbele ya Mlandege kwenye Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, uongozi wa timu hiyo umesema bado una imani na kikosi hicho kufanya vizuri mechi zijazo.
Katika msimu wa 2024-2025, kikosi hicho kilichokuwa chini ya kocha mkuu Ame Msimu, kilibeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) mbele ya mabingwa watetezi, Chipukizi, mechi ya fainali iliyochezwa Juni 21, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.
Licha ya timu hiyo kubeba taji hilo, haikuwa na ubora kama ilivyokuwa awali jambo ambalo lilisababisha kumaliza Ligi Kuu Zanzibar katika nafasi ya 12 ikivuna pointi 39 kwenye mechi 30 ilizocheza.
Wakati timu hiyo ikijiandaa na msimu huu ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, uongozi ulifanya uamuzi wa kumuongeza kocha Hababuu Ali ili kuongeza nguvu katika benchi la ufundi baada ya kocha Ame kutokidhi vigezo vya CAF.
Hadi kufikia sasa, timu hiyo imeshacheza mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar ikivuna alama moja tu na kushika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi hiyo.

Wakati kwenye ligi hali ikiwa hivyo, kikosi hicho kinajiandaa kucheza hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanya vizuri hatua ya awali kwa kuiondosha AS Port ya Djibouti kwa mabao 4-2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali amesema bado ana matumaini na kikosi chake, huku akitaja sababu kuu mbili ambazo zinampa jeuri ya kusema hivyo.
Ametaja sababu hizo kuwa ni kutwaa Ngao ya Jamii msimu huu mbele ya mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege na kuvuka hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Sababu hizi zinanipa nguvu na ari ya kusema kwa kinywa kipana kuwa KMKM ni timu nzuri na mabadiliko yanaonekana hata mashabiki wanapata hamasa ya kufika uwanjani kuishangalia timu hii,” amesema Hababuu.

Pia, amesema anavutiwa na timu hiyo kwa wachezaji wengi kuwa na nidhamu ingawaje wachache bado hawajajitambua lakini hilo analichukulia kama changamoto ya kuifikisha timu hiyo sehemu salama.
Ameeleza hali ya timu hiyo kupoteza mechi itawajenga wachezaji kisaikolojia kwa kutambua wanapaswa kucheza kwa tahadhari.