Kadi nyekundu zatawala KVZ ikiitandika KMKM

TIMU ya KVZ, imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) iliyochezwa Oktoba 7, 2025 kwenye uwanja wa Mao A uliopo Unguja, huku timu zote zikiambulia kadi nyekundu.

KVZ imeibuka na ushindi huo baada ya kutoa sare katika mechi ya kwanza, huku Mabaharia wakipoteza na kuambulia alama moja pekee katika mechi mbili baada ya awali kutoka sare na Mlandege.

Samson Kakwala aliitangulizia bao KVZ dakika ya 36 ambapo ilifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiongoza. Kipindi cha pili dakika ya 55, Michael Joseph alipiga kichwa kilichokubali nyavuni kwa kuwapoteza beki na kipa wake. Katika mechi hiyo, zilionyeshwa kadi tatu nyekundu huku mbili zikienda kwa KVZ na moja KMKM.

Ligi hiyo iliyoanza Septemba 25, 2025, imeshuhudiwa ushindani mkubwa ambapo Oktoba 4, 2025, Uhamiaji iliichapa Mwembe Makumbi mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Mao A. Wafungaji wa Uhamiaji ni Ali Khatib dakika ya 18, Abel Semwiga (dk 31), Ismail Haji (dk 60) na Mohamed Mussa (dk 70).

Mechi mbili zilizochezwa Oktoba 5, 2025, Kipanga ilisulubu New Stone mabao 2-0, huku Mafunzo ikitoa sare dhidi ya Fufuni kwenye uwanja wa Mao A, Mjini Unguja. Oktoba 6, 2025, Polisi ilibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya New King.