ALIYEKUWA Kocha wa Pamba Jiji na Coastal Union, Mkenya, Yusuf Chippo, amesema sababu za kuvutiwa kurejea kufundisha katika soka la Tanzania ni kutokana na maendeleo makubwa yaliyopo, tofauti na nchi nyingi za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu Agosti 21, 2025, yupo katika hatua za mwisho kujiunga na Mtibwa Sugar kwa ajili ya kuiongoza timu hiyo kwa msimu huu 2025-2026 akishirikiana na Awadh Juma ‘Maniche’ aliyeipandisha daraja kushiriki Ligi Kuu Bara.
“Ukiangalia ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania imepiga hatua kubwa sana kisoka ndio maana hatushangai kuona wachezaji na hata makocha wengi kutoka mataifa makubwa wakija hapa, kiukweli ni ligi inayovutia sana kufanya kazi,” amesema Chippo.

Chippo amesema licha ya fursa mbalimbali zinazopatikana katika Ligi Kuu Bara, presha ni kubwa pia kutokana na mahitaji ya kila timu, ingawa hashangai kwani fedha zinazotumika kuanzia maandalizi ni nyingi na ni lazima ziendane na matakwa hayo.
Kocha huyo anakumbukwa na mashabiki wengi hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.
Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu 2025-2026 ikiwa ndio bingwa wa Ligi ya Championship 2024-2025 baada ya kumaliza kinara kwa pointi 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja msimu wa 2022-2023.
Timu hiyo imecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara hadi sasa ikiwa chini ya Maniche, ambapo ilianza kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Mashujaa Septemba 21, 2025, kisha kushinda mabao 2-0, mbele ya Fountain Gate Septemba 28, 2025.

Kibarua cha kwanza kwa Chippo, kitakuwa mechi ya Oktoba 19, 2025, nyumbani dhidi ya Coastal Union, huku timu zote zikiwa na makocha wapya, baada ya ‘Wagosi wa Kaya’, kumtambulisha kocha Mohamed Muya aliyerithi nafasi ya Alli Mohammed Ameir.