BADO WATATU – 51 | Mwanaspoti

TULIPOSHUKA kwenye gari alituonyesha chumba chake.

“Hivi vyumba vingine wanaishi kina nani?” nikamuuliza.

“Vina wapangaji wengine. Chumba changu mimi ni kimoja tu.”

“Sasa tufungulie mlango. Tunataka tufanye upekuzi.”

 “Lakini mimi si jambazi na si mwizi. Mimi ni muuaji tu,” kijana huyo akaniambia — kauli ambayo ilinishangaza.

“Kwani nani alikwambia wewe ni jambazi au mwizi?” nikamuuliza.

“Sasa, mnataka mfanye upekuzi wa kitu gani chumbani kwangu?”

“Upekuzi ni kitu cha kawaida kwa mhalifu yeyote, hata kama si jambazi au mwizi. Tunakipekua chumba chako kwa mujibu wa sheria zetu. Tunaweza kupata kitu ambacho huruhusiwi kuwa nacho.”

“Mimi sina kitu chochote ambacho si ruhusiwi kuwa nacho,” akajibu.

“Unajua kuua ni uhalifu mkubwa. Huwezi kuwa muuaji mpaka uanze na uhalifu mdogo mdogo. Tuna shaka kwamba unaweza kuwa na vitu visivyo vya kawaida.”

“Sawa. Nitawafungulia mpekue, lakini ninakuhakikishia kuwa sikuwahi kuwa mhalifu mdogo hata siku moja.”

Nilishangaa jinsi yule kijana alivyokuwa akijiamini na kuuliza maswali, japokuwa alikuwa amezungukwa na polisi.

Alitufungulia mlango, akatukaribisha chumbani mwake kama vile anakaribisha wageni wake. Tuliingia na kukiona chumba chake kidogo ambacho hakikuwa na kitu chochote zaidi ya kitanda na meza ndogo iliyokuwa na jiko la kutumia mafuta ya taa.

Upande mmoja wa ukuta wa chumba hicho alikuwa ametundika suruali moja na mashati mawili.

Kwenye dirisha palikuwa na mswaki na dawa ya kusafisha meno pamoja na sabuni ya kuogea.

Kukipekua chumba cha aina hiyo ilikuwa kazi ndogo sana kwa sababu hakukuwa na sehemu za kificho. Ilituchukua robo saa tu kukipekua na, kama alivyosema yeye mwenyewe, hatukukuta kitu chochote kisicho cha kawaida; sehemu za kupekua zilikuwa mvunguni mwa kitanda na chini ya godoro. Hakukuwa na sehemu nyingine.

Chini ya godoro lake tulikuta shilingi elefu tisini ambazo alituambia tuziache.

“Hamna kitu kingine,” nikasema baada ya upekuzi huo.

“Niliwambia,” Kijana huyo akaniambia.

“Sasa tunarudi kituo cha polisi.”

Tukatoka katika kile chumba. Kijana huyo alifunga chumba chake kwa funguo tukaondoka.

Tuliporudi kituo cha polisi nilimpeleka katika ofisi ya Sajin Meja Ibrahim akachukuliwa alama zake za vidole.

“Afisa upelelezi anataka ajue kama hana rikodi yoyote ya uhalifu iliyoko mikononi mwetu. Kwa hiyo utazifanyia uchunguzi,” nikamwambia sajin meja huyo.

“Sawa afande, nitashughulikia.”

Baada ya hapo  nikaenda kumuweka kijana huyo mahabusi.

Wakati nipo ofisini kwangu afisa upelelezi akanipigia simu.

“Umeyafanyia kazi maagizo yangu?” akaniuliza mara tu nilipopokea simu yake.

“Ndiyo afande. Tumekwenda kupekua chumba chake, hatukupata kitu chochote na alama za vidole vyake zimeshachukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.”

Afisa upelelezi alipojibu hivyo akakata simu. Nikaendelea na kazi zangu hadi saa saba nilipotoka kwenda kwenye mkahawa kupata chakula cha mchana. Nilipomaliza kula nikarudi tena ofisini. Nilifanya kazi hadi saa tisa mchana nilipoondoka kurudi nyumbani.

Siku ile ikapita. Asubuhi iliyofuata ndipo mama yake Faustin alipofika kituoni. Aliletwa ofisini kwangu na polisi aliyekuwa kaunta.

Nilimkaribisha kwenye kiti na kuanza kuzungumza naye.

“Nimefika jana usiku nimelala gesti,” akaniambia.

“Pole kwa safari na nimefurahi kuwa umekuja.”

“Nimekuja haraka kwa sababu nimeshituka kutokana na hii taarifa ya mwanangu.”

“Mwanao tuko naye. Hivi ulivyokuja utatusaidia kutupa taarifa zaidi za mtoto wako kuhusu maisha yake tangu akiwa mikononi mwako. Ninataka utuambie tabia yake ikoje.”

“Mbona mwanagu ni kijana mpole tu, hili tukio nililoelezwa mpaka sasa siamini kama amefanya hivyo kweli.”

“Mwenyewe si amekueleza?”

“Amenieleza ndiyo lakini bado siamini.”

“Faustin hajawahi kushiriki katika uhalifu mdogo mdogo kama  vile kupora watu, kupiga watu na vitu kama hivyo…”

Mwanamke alikuwa akitikisa kichwa kukataa hata kabla sijamaliza nilichokuwa ninasema.

“Hakuwahi…hakuwahi hata siku moja. Mpaka sasa najiuliza huo ujasiri wa kunyonga watu aliupata wapi.”

“Jinsi alivyouandaa mpango wa kuwanyonga wale watu na mwenyewe kujihami ni kitu ambacho hadi sasa tunajiuliza alipata wapi uwezo ule ambao hutumika na wahalifu wakubwa.”

“Labda kama kulikuwa na watu waliomshawishi na kumsaidia. Kama unavyomuona mwenyewe, mwanangu ni mdogo sana.”

“Amesema hakushirikiana na mtu yeyote. Ameua kwa akili yake na huo mpango aliupanga mwenyewe.”

“Inawezekana kweli hasa ukiangalia umri wake?”

“Ndio tunajiuliza na tunaamini wewe unaweza kutusaidia kwa sababu ndiye unayezijua tabia zake vizuri.”

“Ninachosema mimi ni kwamba mwanangu hawezi kufanya kitendo kama hicho. Hicho kitendo kinataka mtu katili wakati mwanangu si katili. Ni mpole sana. Imani yangu ni kwamba yuko mtu au watu wengine ambao wamefanya kitendo hicho. Sasa wamemtoa muhanga mwanangu.”

“Sasa tumtoe mahabusi umuhoji wewe mwenyewe.”

Nikapiga simu kaunta kuwambia polisi wamtoe Faustin na kumleta ofisini kwangu.

Baada ya dakika tatu tu Faustin akaingizwa ofisini kwangu. Alipomuona mama yake alishituka.

“Marahaba. Nimekuja Tanga kwa ajili  yako Faustin. Hebu niambie ukweli kama ni wewe uliyewanyonga wale watu?”

“Niliwanyonga mimi,” fausitin alimjibu bila kusita.

“Ndiyo, mimi mwenyewe.”

“Mimi siamini. Wewe huna uwezo huo labda kama kuna watu ulioshirikiana nao.”

“Sijashirikiana na mtu yeyote na wala sijamueleza mtu yeyote siri hii.”

“Sema ukweli mwanangu kama kuna watu wamekutoa mhanga.”

“Hakuna watu walionitoa mhanga mama yangu.”

“Kwa hiyo uko tayatri upelekwe mahakamani peke yako?” Nikamuuliza Faustin.

“Kama huko tayari kupelekwa mahakamani peke yako, taja na wenzako ulioshirikiana nao.”

Faustin akatikisa kichwa bila kusema chochote.

“Hutaki kuwataja?” mama yake akamuuliza.

Faustin aliendelea kutikisa kichwa.

“Maana ya kusema hawapo ni kwamba sijashirikiana na mtu yeyote.”

Ghafla nikamuona mama yake Faustin akiangua kilio. Nikahisi ni huzuni zilizotokana na kitendo alichokifanya mwanawe.

“Usilie. Tusubirie hukumu ya mahakama,” nikamwambia mwanamke huyo na kuongeza.

“Mwanao anakiri kosa lake yeye mwenywe.”

“Mama nyamaza usilie…” Faustin alimwambia mama yake huku akimshika bega.

“Tumpe funguo ya nyumbani kwako,” nikamuuliza Faustin.

“Mpe,” Faustin alinijibu kisha akamtazama mama yake.

“Mama utakwenda kulala chumbani kwangu.”

Mama yake alijifuta machozi kisha akamwambia mwanawe.

“Sijui unaishi wapi.”

“Tutakupekea nyumbani kwake,” nikamwambia mwanamke huyo.

“Chini ya godoro kuna hela zangu shilingi elfu tisini, utatumia” Faustin akamwambia mama yake..

Maneno yake yakamfanya mwanamke huyo  aendelee kulia huku akijisemea pake yake.

“Sijui mwanangu umepatwa na balaa gani wewe!”

Nilipoona mwanamke huyo anazidi kulia nilimuagiza yule polisi amrudishe Faustin mahabusi kisha nikatoka na mwanamke huyo. Nilimpakia kwenye gari na kumpeleka Pongwe katika nyumba anayoishi Faustin.

“Faustin anaishi hapa.” nikamwambia mwanamke huyo baada ya kushuka kwenye gari.

Mwanamke huyo ambaye alikuwa ameshanyamaza kulia akaniuliza.

“Chumba chake ni kipi?”

Nilimuonesha chumba cha Faustin na kumpa funguo afungue  mlango.

Mwanamke huyo alifungua mlango na kukichungulia chumba hicho kisha akageuka na kuniuliza.

“Wewe huingii ndani?”

“Nimekuleta wewe ili usiendelee kukaa gesti.”

Wakati nazungumza na mwanamke huyo mlango wa chumba cha pili ulifunguliwa. Akatoka mwanamke mmoja aliyekuwa amejifunga khanga kifuani na nyingine kiunoni. Akatusalimia.

“Habari ya saa hizi jamani?”

Tukamjibu kuwa ni nzuri. Mama yake Faustin ndiyo aliendelea kuulizana naye hali.

“Naona umefanana na Faustin!” Yule mwanamke akamwambia mama yake Faustin.

“Ni kweli. Faustin ni mwanangu. Nimekuja jana kutoka Lindi.”

“Na Faustin mwenyewe sijamuona tangu jana!”

“Faustin yuko polisi ndiyo maana mimi nimekuja hapa.”

“Amefanya nini tena?”

“Ni matatizo tu ya kidunia. Huyo kaka naye ni polisi, ndiye aliyenileta hapa nyumbani ili nikae hapa wakati nafuatilia habari za mwanangu.”

Mwanamke huyo akanitazama tena sasa akiwa na uso uliotaharuki.

“Sijakutambua kwa sababu umevaa kiraia. Karibuni sana,” akaniambia.

“Tumeshakaribia. Nimefurahi kwamba tumekutana na mwenyeji wa hapa. Msije mkamshangaa huyu mama, ni mama yake Faustin na Faustin mwenyewe yuko mikononi mwetu.”

“Sawa kaka, hakuna tatizo. Mgeni tumeshamuona, tutakuwa naye.”