EQUITY BANK YAAHIDI KUENDELEA KUPANUA HUDUMA ZA KIFEDHA KUPITIA UBUNIFU WA KIDIGITALI

::::::::

Benki ya Equity Tanzania imeahidi kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidigitali, kupanua matawi na kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Isabella Maganga, amesema Equity inaendelea kuimarisha ubunifu ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora na nafuu zaidi kupitia njia za kidigitali na matawi mapya yatakayofunguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Maganga amesema kaulimbiu ya mwaka huu, “Mission is Possible,” inaakisi dhamira ya benki hiyo katika kuwawezesha wateja wake kufikia mafanikio ya kifedha na kibiashara,amesisitiza kuwa benki imekuwa mstari wa mbele katika kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia bidhaa rafiki zisizo na makato makubwa, ambazo zinamwezesha Mtanzania wa kipato cha chini kupata huduma za kibenki kwa urahisi zaidi.

Kwa upande wake, Prosper Nambaya, Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank Tanzania, amesema benki hiyo inaendelea kupanua mtandao wake wa huduma kwa kuongeza matawi mapya, kuimarisha huduma za internet banking, na kuongeza mawakala wa kibenki hadi kufikia zaidi ya 3,000 nchi nzima,ameongeza kuwa mpango wa kufikia mwaka 2030 ni kuwa na angalau matawi 55, sambamba na ushirikiano mpya wa Umoja Switch utakaowawezesha wateja kutumia zaidi ya mashine za ATM 1,000 kote nchini.

Wateja wa benki hiyo pia wameelezea kuridhishwa na huduma za benki hiyo Uinde Muro, Mkurugenzi wa Imperium OpEx, amesema benki hiyo imemsaidia kukua kibiashara kwa kuwa na huduma zinazojali mahitaji ya mteja huku Benson Maenya, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya GSM, amesema Equity imekuwa mshirika muhimu katika kupanua biashara zake ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki, kutokana na mtandao mpana wa kimataifa na huduma bora kwa wateja.