Mgombea UDP aahidi neema kwa wajasiriamali Pemba

Pemba. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha United Democratic Party (UDP), Saumu Hussein Rashid amewahidi wafanyabiashara na wajasiriamali kuwapa mazingira bora ya biashara ili kufanya shughuli zao kwa wepesi na tija zaidi.

Mgombea huyo ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 8, 2028 alipotembelea Soko la Tibirinzi, Chakechake Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kampeni zake.

Saumu  amesema iwapo akipata ridhaa ya uongozi atawapatia mikopo yenye masharti nafuu ili kila mfanyabiashara akuze biashara zake na kuingia katika pato la Taifa.

Pia, amesema lengo la UDP ni kufungua fursa za kiuchumi ili kila Mtanzania awe na uchumi imara na kipato cha kujitosheleza.

Amesema wajasiriamali wengi wanashindwa kukuza biashara zao kutokana na kukosa mitaji ya kuendesha biashara zao,  hivyo atakapopata ataweka mazingira rafiki kwa kila mfanyabiashara kupata mitaji ya kukuza kazi zao litakalowawezesha kujikwamua kimaisha.

“Nawaahidi mtakaponichagua nitaweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara zenu nitawapambania kupata mikopo yenye masharti nafuu kuona kila mfanyabiashara anaweza kuchukua mikopo hiyo,’’amesema Saumu.

Aidha, Saumu amesema mbali ya kuondosha changamoto ya mitaji pia atafanya punguzo katika suala la kodi ili kuwapa unafuu wafanyabiashara hao na kupunguza ukali wa maisha.

“Jambo jingine la kodi,  mmekuwa mnalalamikia kodi wakati mkisafirisha biashara zenu nitapunguza kwa kiasi kikubwa ili mpate wepesi na kuimarisha biashara zenu,’’amesema Saumu.

Mgombea huyo, amesema atajenga viwanda kila mkoa kulingana na shunguli za kiuchumi katika eneo husika, kuona kila mwananchi anapata fursa ya kujipatia kipato.

Amesema kwa vile wananchi wa Pemba, wana uhusiano wa karibu na wa Tanga katika Shughuli za kibiashara, hivyo atatengeneza miundombunu ya bandari na kuleta boti za kisasa zitakazorahisisha ufanyaji wa biashara zao.
Ali Khamis Ali, mfanyabiashara katika Soko la Tibirinzi, amemuomba mgombea huyo kuliangalia kwa karibu suala la kodi kwa kuwa linawakwaza katika ufanyaji wa biashara zao.

Ameeleza kuwa, anaamini watakapondoshewa au kupunguzia kodi na kupatiwa mitaji, wanaweza kupiga hatua kubwa kujikwamua kimaisha.

Mfanyabiashara mwingine, Muhammed Juma Rehan ameomba mgombea huyo kuwajengea soko jumuishi la kisasa litakalokusanya biashara zote kwenye soko hilo.

“Haiwezekani mtu anakuja kutafuta bidhaa hapa ananunua samaki, lakini bidhaa nyingine afuate kwenye soko lingine huo utakuwa ni usumbufu kwao,” amesema.

Mapema mgombea huyo baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa Pemba alifika katika Kijiji cha Wawi na kuzuru kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Omar Ali Juma na kumtakia dua.

Pia, amesema chama hicho kinathamini juhudi za waasisi wa nchi hii waliotangulia mbele ya haki kutokana na kazi kubwa walioifanya katika ujenzi wa Taifa hili.