CCM kujenga Makumbusho ya Historia ya Z’bar, Dk Nchimbi amtaja OMO

Pemba. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi ujenzi wa makumbusho ya historia ya Zanzibar katika kipindi cha miaka mitano.

Pia, amesema CCM chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar wakipata ridhaa ya wananchi Oktoba 29, 2025 kuwatumikia, wataulinda na kuudumisha muungano kwa gharama zozote.

Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 8, 2025 katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika, Mkoa wa Kusini Pemba, Uwanja wa Mpira Kinyansini, Jimbo la Gando.

Amesema pamoja na mambo mengi na ambayo yanakwenda kufanyika miaka mitano ijayo ni ujenzi wa makumbusho ya Zanzibar yatakayokuwa na historia mbalimbali ikiwemo Mapinduzi ya visiwa hivyo yaliyotokea Januari 12, 1964.

“Tunakwenda kujenga makumbusho ya Zanzibar itakayokuwa na historia ya Zanzibar, Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, Historia ambayo imemkomboa Mzanzibar, Historia ambayo imeleta usawa miongoni mwa Wazanzibar,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema leo Wazanzibar wamekuwa kitu kimoja, Watanzania wamekuwa wamoja kitu ambacho kinapaswa kujivunia.

Dk Nchimbi amesema wataziimarisha taasisi zote za umma za Muungano ili ziweze kuwatumikia wananchi kwani zina wajibu wa kuleta matunda kwa Taifa na wananchi.

Akigusia ushindi wa CCM Pemba ambayo kwa miaka mingi ni ngome ya upinzani, Dk Nchimbi amesema:”

Nataka niwaambie, dalili ni kwamba chama chetu hapa Pemba kitapata ushindi wa kishindo, mambo ambayo yamefanywa na Rais Samia na Dk Hussein Mwinyi ni makubwa kwenye nyanja zote.”

Amesema kasi ya kukuwa kwa uchumi wa Zanzibar umefikia asilimia saba, mkubwa kabisa na hii ni kwa ushirikiano wa wananchi wa Zanzibar.

“Leo wana CCM wanaona fahari kujinasibu na viongozi wetu hawa, viongozi hawa hawana makuu, hawana makeke kwani kazi zao zinaonekana. Hatulazimiki kuongea hadi asubuhi kwani kazi zao zinaonekana,” amesema Dk Nchimbi.

Mgombea mwenza huyo amesema

kubwa kuliko yote yaliyofanyika ni umoja wa Watanzania na Wazanzibar. Tunu za Taifa zimelindwa vyema.

“Viongozi wetu wameendeleza kudumisha amani na usalama katika nchi yetu. Tumesema kwenye ilani yetu kwamba jambo kubwa tutakalolifanya kwa wananchi ni kudumisha usalama wao, amani yao, kuishi kindugu na kusaidiana,” amesema.

Akisisitiza, Dk Nchimbi amesema: “Tutaendelea kuulinda Muungano kwa gharama yoyote kwa sababu tunasema umoja ni nguvu, muungano wetu ni wa undugu na lazima tuulinde.”

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amewaomba wana CCM kuzisaka kura kwa wananchi hata wasio wa chama hicho zikiwamo za Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, maarufu OMO.

OMO ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na katika uchaguzi mkuu huu yeye ni mgombea urais wa Zanzibar akichuana vikali na Dk Mwinyi.

“Kampeni za CCM zimekuwa rahisi kwa sababu Mama Samia amefanya kazi kubwa. Ni mama wa mfano na angalieni mikutano yake, kila anapokwenda anaambiwa unawadai.

Hapa Wapemba fikisheni salamu, kama kuna kitu dunia itatushangaa basi ni kumpa kura chache,” amesema.

Huku akishangiliwa na matarumbeta yakipigwa, Dk Nchimbi akasema:”

Hata walio karibu na OMO, nendeni mkamwombe kura, kwa kazi kubwa iliyofanyika mwambieni tunaomba kura na ombeni kwa heshima.

Asitukanwe mtu, asidhalilishwe mtu, mwambieni Mzee kazi aliyofanya Rais Samia umeiona, kazi aliyoifanya Dk Hussein Mwinyi umeziona, tunaomba kura yako,” amesema.

Dk Nchimbi amesema chama hicho kimejizatiti kuendeleza maridhiano: “Mafanikio ya Rais Mwinyi kudumisha upendo lazima yalindwe na yapendwe na hata kitaifa, ndani ya siku 100 tukipewa ridhaa, Rais wetu Samia amesema tutaunda Tume ya Maridhiano ili kila mmoja asikilizwe.”

Akimzungumzia Dk Mwinyi, mgombea mwenza huyo amesema: “Mimi sina mashaka na uwezo wa Dk Mwinyi, alipokuwa Waziri wa Ulinzi, mimi nilikuwa naibu waziri wake kwa miaka mitatu. Najua uwezo wake.”

“Changamoto pekee aliyonayo, hawezi kujigamba gamba, lakini kila mmoja ameona maendeleo aliyoyafanya,” amesema.

Katika miaka mitano, Pemba wanakwenda kuweka mkazo na uwazi wa kuimarisha na kuboresha kilimo cha umwagiliaji ambacho kimekuwa visiwani humo.

Amesema katika kuhakikisha hilo, mbegu, mbolea na mikopo inapatikana ikiwamo masoko.

Karafuu, matunda na mbogamboga zinalimwa kwa wingi.

“Miaka mitano ijayo, Tumejizatiti kuimarisha uchumi wa buluu, Ilani ya 2020 iliongelea kuwa na uchumi lakini sera za Rais Mwinyi alikuja na uchumi wa buluu. Pia, tunakwenda kuboresha bandari ya Wete, lakini kuimarisha ufungaji wa samaki, kuimarisha kilimo cha mwani,” amesema.

Amesema wamedhamiria katika eneo la uvuvi, kuongeza kasi kwani kwa sasa tunazalisha tani 80,000 kwa mwaka, miaka mitano Zanzibar izalishe tani 160,000.

Amesema miundombinu ya mawasiliano nayo tunakwenda kuiboresha ikaiwamo kuboresha uwanja wa ndege wa Pemba ili uwe uwanja wa kimataifa na tukifanikiwa ndege zenye ukubwa mbalimbali zitatua Zanzibar, idadi ya mizigo itaongezeka n ndege za watalii zitaongezeka.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Aboud Mohamed amesema anamfahamu Dk Nchimbi kwani amefanya naye kazi kwa kipindi kirefu: “Ni mtu mwadilifu, mcheshi, mpenda watu na ni mtu anajua Watanzania wanataka nini, nataka niwahakikishie atakuwa mshauri mzuri sana wa mama yetu, Samia Suluhu Hassan.”

Aboud amesema: “Dk Nchimbi nataka nimwambie, Pemba ya leo ni Pemba mpya, Pemba ya CCM, yale ya zamani yamepita, wananchi hapa wapo tayari kukipigia kura Chama cha Mapinduzi.

Sasa Pemba imetulia, hakuna ugomvi ugomvi, hakuna maneno maneno, tunasubiri Oktoba 29 tukipe kura. Nilikuwa naomba kuwa na umoja wa Ugunja na Pemba,” amesema.

‘Tupeni tena tuwawakilishe’

Mgombea ubunge wa Gando, Salum Mussa Omary amesema Oktoba 29, tunakwenda kuzivua kura za Rais Samia, Dk Mwinyi, zangu na wananchi wanasema tunakwenda kushinda kwa kishindo.

 Naye Mwakilishi wa Jimbo la Gando, Wilaya ya Wete, Mariam   Juma amesem: “Mmeona juhudi kubwa ya Rais Mwinyi aliyoyafanya, barabara, hospitali zimejengwa, kuna shule za ghorofa na za chini zimejengwa, sasa tunataka nini tena.

Zanzibar ya leo si ya zamani, hatuna budi kulipa fadhila za yale waliyoyafanya Oktoba 29.”

Kwa upande wake, Kada wa CCM aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum  Chadema, Cecilia Pareso .amesema: “Chama cha Mapinduzi kimetuletea viongozi wenye sifa za kipekee na kwenye nafasi ya urais, imetuletea mwana mama mzalendo, mpambanaji na shupavu kwelikweli.

Tukampigie kura za kishindo na za heshima. Kina baba na vijana nanyi twendeni tukapige kura kwa Samia, Dk Mwinyi, wabunge na madiwani wote ili kwa pamoja hii timu ikatuletee maendeleo,” amesema.