Mwanza. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuimarisha sekta nne muhimu za maendeleo ambazo ni kilimo, afya, elimu na miundombinu huku akisisitiza hatua hiyo itaifanya kanda ya ziwa kuwa kitovu cha biashara nchini.
Akihutubia mkutano wa kampeni leo Jumatano Oktoba 8, 2025, uliofanyika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza, Samia ameahidi Serikali atakayoiongoza endapo atapewa ridhaa, itaweka mkazo mkubwa katika kuongeza uzalishaji na kuvutia uwekezaji.
Akizungumzia sekta ya kilimo, mgombea huyo amesema tayari Serikali imeagiza matrekta 700 na kati ya hayo, 350 yameshawasili nchini na yatasambazwa kwa wakulima kupitia vituo vya zana za kilimo vitakavyojengwa kwenye kanda mbalimbali.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wakulima, hususan wa pamba katika kanda ya ziwa, kulima kwa gharama nafuu.
“Tumekwishasambaza mbegu na dawa za pamba bure, si kwa ruzuku. Vilevile, tumeajiri vijana 700 wa huduma za ugani ili kuongeza ufanisi wa kilimo,” amesema.
Aidha, Samia ameahidi kufufua viwanda katika maeneo ya Sengerema, Buchosa na Manawa (Misungu), pamoja na kufufua Chama Kikuu cha Ushirika cha Mwanza.
Mgombea huyo amesema Serikali yake itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga hospitali mpya ya kibingwa mkoani Mwanza ili kupunguza rufaa kwenda Dar es Salaam, sambamba na kuboresha Hospitali ya Nansio iliyopo Ukerewe.

Miundombinu na nishati
Katika sekta ya barabara, amesema tayari ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Buhongwa–Igoma yenye urefu wa kilomita 14 umekamilika, huku zabuni ya Barabara ya Mwanza–Buhongwa–Usagara yenye njia nne na barabara ya mwendokasi ikiwa imetangazwa. Pia, ameahidi ujenzi wa barabara za wilaya na mitaani kwa lengo la kuunganisha makao makuu ya kata, wilaya na mikoa.
“Lakini Serikali itaendelea kujenga vituo vya kusambaza umeme ili kuhakikisha huduma inapatikana kwa saa 24, Serikali pia itaendelea kuweka kipaumbele katika matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema mgombea huyo wa CCM.
Akizungumzia miradi mikubwa Samia ameitaja itakayochochea uchumi wa Mwanza ukiwamo wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza–Isaka (km 314) ambacho kimefikia asilimia 63 na kugharimu Sh3 trilioni.
“Mwanza itakuwa na stesheni tano za SGR zitakazotoa fursa za biashara, malazi na huduma mbalimbali. Tukimaliza reli hii, safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza itapungua kutoka saa 18 hadi saa 8 au 9 pekee,” ameahidi Samia.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi bidhaa utaongeza ajira na kurahisisha biashara. Aidha, amesema Serikali imewekeza Sh120.6 bilioni katika ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza iliyokamilika kwa asilimia 98.
Amesema meli hiyo inabeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari 20 na malori makubwa matatu kwa wakati mmoja.
Kuhusu uwanja wa ndege wa Mwanza, ameahidi utaboreshwa kuwa wa kimataifa ili kuvutia watalii, hususan wanaoelekea Hifadhi ya Serengeti.
Katika hatua nyingine, Samia ameahidi kuwa Serikali atakayoiongoza itafufua viwanda vya kuzalisha vifaa tiba ikiwamo bandeji, pamba na shuka ambavyo kwa sasa vingine huagizwa nje ya nchi.

Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Dk Bashiru Ali, akizungumza leo Jumatano Oktoba 8, 2025 katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza,katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan
Bashiru alivyomnadi Samia
Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Dk Bashiru Ally akizungumza katika mkutano huo, amesema pamoja na mafanikio makubwa ya uongozi wa Samia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, bado suala la amani ya Taifa linapaswa kupewa uzito wa kipekee.
Dk Bashiru amesisitiza umuhimu wa Watanzania kulinda misingi ya amani na usalama wa Taifa bila kuruhusu hofu au kupoteza mshikamano wa kitaifa.
“Hivi vingine vineno vineno vina watu wamevipanga, ni rahisi kuwadhibiti na anao uwezo huo. Simaanishi tupuuze majaribio ya kutikisa amani na misingi ya usalama wa nchi yetu, hata kidogo. Ninachotaka kusema ni kuwa huyu kiongozi ni hazina ya uongozi katika vipindi vigumu sana,” amesema Dk Bashiru.
Mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi amesema jimbo hilo awali lilikuwa na mtandao wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 34 pekee, lakini katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia, barabara hizo zimeongezeka kwa kilomita 39.
Ameongeza kuwa, maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza yatakuwa chachu ya kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa na kurahisisha safari za kitalii kuelekea Hifadhi ya Serengeti.