Mtoto mbaroni akidaiwa kumuua mama yake wa kambo

Mbeya. Tatizo Mzumbwe (25), mkazi wa Masoko  mkoani Mbeya, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mama  yake wa kambo, Merry Yohana (61) kwa madai ya kumkata na panga kichwani.

Merry mwenye ualbino, amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kukatwa na panga kichwani, kufuatia mzozo wa kugombea mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na marehemu mumewe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa kwa kina kuhusu tukio hilo.

Kuzaga amedai kuwa, mtuhumiwa alitenda kosa hilo Oktoba 6, 2025, saa 2:00 asubuhi nyumbani kwao katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Masoko kwa kumshambulia Merry kwa panga kichwani na kusababisha kumwagika kwa damu nyingi.

Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia uliotokana na mashamba yaliyokuwa ya marehemu mume wa Merry ambaye pia alikuwa baba mzazi wa mtuhumiwa.

“Awali, mtuhumiwa alikuwa akimshinikiza  kugawana mashamba ya urithi  yaliyoachwa na  baba yake  jambo ambalo marehemu  akakubaliana nalo, ndipo alijichukulia sheria mikononi na kutekeleza  mauaji hayo,” amesema Kuzaga.

Amedai mtuhumiwa alitumia panga kumshambulia  Merry  na kusababisha  kutokwa damu nyingi  iliyokuwa sababu ya kifo.

Katika hatua nyingine, Kuzaga ameonya jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi kutokana na migogoro  ya kifamilia kwa  kugombea mali badala yake kutafuta njia mbadala ya kupata mwafaka.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa baadhi  ya vijana kuacha tamaa ya kujipatia mali kinyume cha sheria na kueleza kuwa mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa kwa uchunguzi  zaidi na atafikishwa mahakamani wakati  wowote,” amesema Kuzaga.

Baadhi ya wakazi wamekemea kitendo hicho cha mauaji na kuliomba  Jeshi la Polisi kufanya mahojiano zaidi na mtuhumiwa huenda lengo la tukio hilo  halikuwa mgogoro  wa mashamba.

Telezia Joel, ameshauri  Serikali  kuweka mfumo wa utoaji elimu kwa  makundi rika sambamba na wanaoingia kwenye ndoa.