Morogoro. Taharuki imezuka miongoni mwa wakazi wa Kitongoji cha Bwawani, Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa, kufuatia taarifa za kutoweka kwa mfanyabiashara wa huduma za kifedha, Rogers Yohana Ludovick (34), katika mazingira yanayodaiwa kuwa ya utata.
Tukio hilo liliripotiwa kutokea jana majira ya saa saba mchana, na taarifa za kutoweka kwake zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii muda mfupi baada ya tukio hilo, jambo lililochochea hofu na wasiwasi kwa wakazi wa eneo hilo na familia yake.
Hadi sasa, haijafahamika aliko mfanyabiashara huyo, huku juhudi za kumtafuta zikiendelea kushirikisha vyombo vya usalama pamoja na jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Alex Mkama, amethibitisha leo, Oktoba 8, 2025, kuwa Jeshi la Polisi limepokea taarifa za kutoweka kwa mfanyabiashara huyo, na tayari limeanza uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hili, tunawaomba wananchi kuwa watulivu wakati wa uchunguzi ukiendelea na yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia apeleke taarifa hizo ili zifanyiwekazi,” alisema Mkama.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, mdogo wa Rogers, Abuubakar Yohana Ludovick, amesema kuwa siku ya jana, Oktoba 7, 2025, majira ya saa saba mchana, kaka yake alichukuliwa kwa njia za utata na watu watatu waliotembelea duka lake lililopo Bwawani.

Picha ikionesha eneo analofanyia biashara yake ya miamala ya fedha Rogers Ludovick ikiwa imefungwa tangu jana alivyotoweka katika mazingira ya utatanishi. Picha na Jackson John
Ludovick amesema watu hao walifika kwa gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, kisha kumchukua kaka yake na kuondoka naye kwenda mahali pasipojulikana.
Akisimulia kilichotokea, Ludovick amesema kuwa kabla ya tukio hilo, walimwona kijana asiyejulikana akizunguka mara kadhaa karibu na duka la kaka yake, kana kwamba alikuwa anafanya doria.
Ludovick amesema muda mfupi baadaye, gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe lilipita eneo hilo majira ya saa saba mchana, kisha baada ya dakika chache likarudi tena na kusimama nje ya duka la Rogers.
“Watu wawili walishuka kutoka kwenye gari, mmoja alikuwa amevaa nguo nyeusi akiwa na mwili mkubwa mwingine alikuwa wa kawaida akiwa amevaa shati la mikono mifupi, yule mwenye mwili mkubwa alielekea moja kwa moja dukani na kuanza kuzungumza na kaka.
“Hatukusikia walichoongea, baada ya muda kidogo kaka alitoka nje, akaingiza benchi la wateja ndani kisha yule kijana aliyekuwa akizunguka awali akafungua mlango wa gari kaka akaingia wakafuata wale wawili kisha gari likaondoka,” amesema Ludovick.
Amesema mara baada ya tukio hilo kutokea alijaribu kumpigia simu Rogers bila mafanikio na hadi sasa hawajafanikiwa kufahamu alipo ndugu yao.
Ludovick amesema baada ya hapo aliungana na ndugu wengine wa familia waliokuwa karibu hadi nyumbani kwa kaka yake ambapo walimkuta mkewe na kumulizia kama anataarifa yeyote kuhusu mumewake lakini hawakuweza kufanikiwa kupata chochote kwa sababu naye alikuwa hafahamu kinachoendelea.
Amesema kuwa siku tatu kabla ya tukio, gari hiyo ilikuwa ikionekana mara kwa mara katika mitaa ya Dumila, ingawa hakulipa uzito mkubwa wakati huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bwawani, Ally Omari Abdallah, alithibitisha kutoweka kwa Rogers, akisema anamfahamu kama mfanyabiashara wa miamala ya fedha hajawahi kuhusishwa na migogoro au masuala ya kisiasa.
“Tangu namfahamu Rogers sijawahi kumuona akijuhusisha na masuala ya kisiasa wala sijapokea taarifa ya kuwa na mgogoro na mtu yeyote yule, ni mtu ambaye yupo bize na biashara zake na tukio hili limetushangaza sisi wote wananachi wa Bwawani,” amesema Abdallah.