TAEC Yafanya Ukaguzi wa Matumizi Salama ya Mionzi Katika Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imekamilisha ukaguzi wa matumizi salama ya mionzi katika vituo 66 vinavyotoa huduma za mionzi katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi. Lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha kuwa matumizi ya mionzi yanazingatia usalama wa wafanyakazi wanaoshughulika na vyanzo vya mionzi, wananchi pamoja na mazingira.

Akizungumza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi mara baada ya ukaguzi, Mkaguzi wa Vyanzo vya Mionzi kutoka TAEC, Bi. Lucy Lwai, alisema kuwa ukaguzi huo ni muhimu ili kujiridhisha kuwa mashine zinazotumika zinafanya kazi vizuri, majengo hayavujishi mionzi, na watumiaji wa mionzi wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi salama ya mionzi.

Katika ukaguzi huo, jumla ya vituo 20 vilibainika kuwa vinatoa huduma za mionzi bila kuwa na leseni halali ya matumizi ya mionzi. Kufuatia hilo, TAEC imetoa onyo kali kwa vituo hivyo na kuvielekeza kuhuisha leseni hizo kabla ya kuendelea na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Frank Elisha, alisema kuwa hospitali hiyo ndiyo pekee yenye hadhi ya rufaa katika mkoa wa Katavi, na kwamba mashine ya CT-Scan iliyopo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

Aidha, Dkt. Frank ameishukuru serikali kwa uwekezaji wa vifaa vya mionzi katika hospitali hiyo, akieleza kuwa uwepo wa mashine ya CT-Scan umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama na muda ambao wananchi walikuwa wakitumia kusafiri hadi mikoa ya Mbeya au Mwanza kupata huduma hizo.

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ni taasisi ya serikali yenye dhamana ya kusimamia matumizi salama ya mionzi pamoja na kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa.