Dar es Salaam. Wakati uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa mashirika ya umma na kampuni ndani na nje ya nchi ukiongezeka kwa asilimia saba, wadau wa uchumi wamesema jambo hilo linaongeza nguvu kwa mashirika kujitegemea.
Uwekezaji huo kwa mujibu wa ripoti ya mwaka wa fedha 2024/2025 iliyotolewa na ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) umefikia Sh92.29 trilioni Juni 30, 2025 kutoka Sh86.3 trilioni katika mwaka wa fedha 2023/24.
Uwekezaji huo wa Serikali unahusisha mashirika ya umma 255 na kampuni 45 ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache na taasisi za kigeni 10 ambazo kwa pamoja zinatengeneza uti wa mgongo wa mapato yasiyo ya kodi ya Tanzania.
Uchambuzi zaidi unaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano uwekezaji wa ndani umeongezeka kutoka Sh67.01 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh90.61 trilioni mwaka 2024/25, jambo linalodhihirisha utendaji bora na usimamizi ulioboreshwa katika mashirika ya umma.
Hilo limeenda sambamba na kukua kwa thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi za nje ambao ulitoka Sh722.94 bilioni hadi Sh1.68 trilioni.
Akizungumzia suala hilo jana Oktoba 7,2025, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alisema ongezeko hilo linaonyesha juhudi endelevu za serikali katika kuimarisha usimamizi na utawala bora wa uwekezaji wa umma.
“Ukuaji huu wa uwekezaji unaonesha maboresho katika utawala wa mashirika umma, uhusiano wake na malengo ya maendeleo ya Taifa,” alisema Mchechu.
Alitolea mfano wa mashirika makubwa ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la mtaji wa Serikali ikiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), uliorekodi ongezeko la asilimia 29 katika mali halisi, kutoka Sh7.2 trilioni hadi Sh9.3 trilioni.
Alisema kichocheo kikubwa ni uandikishaji wa wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi na ujumuishaji na mifumo mingine ya serikali kama Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pia, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) nao ulionyesha ongezeko la asilimia 13 katika mali halisi kutoka Sh8.12 trilioni hadi Sh9.2 trilioni.
“Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa michango ya wanachama kufuatia ajira mpya na vyeo kwa watumishi wa umma,” alisema.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pia iliripoti ongezeko kubwa la mali halisi lililokuwa kwa asilimia 82 kutoka Sh1.3 trilioni hadi Sh2.36 trilioni ikiwa ni matokeo ya utendaji thabiti wa kifedha na usimamizi mzuri wa akiba.
Mchechu alisema ongezeko la jumla la uwekezaji wa Serikali limechangiwa pia na taarifa za kifedha zilizoboreshwa ambazo sasa zinaonesha thamani halisi ya hisa na mitaji ya Serikali.
“Tumeona pia ongezeko la akiba na faida zilizokusanywa katika mashirika kadhaa, sambamba na kuongezeka kwa faida katika mashirika mengi ya umma,” alisema.
Katika upande wa mapato yasiyokuwa ya kodi alisema taarifa ya OMH inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la asilimia 34 kutoka Sh767 bilioni mwaka 2023/24 hadi Sh1.03 trilioni mwaka 2024/25.
Ukuaji huo ni sawa na asilimia 92 ya lengo la mwaka huku faida kubwa na nidhamu bora ya kifedha katika mashirika ya umma zikitajwa kuwa sababu za ufanisi.
“Utendaji bora wa kifedha wa mashirika ya umma umeongeza mapato kwa Serikali, jambo linaloimarisha dhamira yetu ya kupunguza utegemezi wa mapato ya kodi na kukuza fedha endelevu kwa miradi ya maendeleo,” alisema Msajili wa Hazina.
Kufuatia hilo, Mchechu alisema Serikali itaendelea kuhakikisha ukuaji endelevu wa uwekezaji wake kupitia mageuzi, ufuatiliaji wa karibu na uwajibikaji mkubwa wa mashirika ya umma.
“Ukuaji huu ni ushahidi wa maendeleo tunayoyapata katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta thamani kwa wananchi. OMH itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali kuboresha utendaji, uwazi na mchango wa mashirika ya umma katika uchumi wa taifa,” alisema.
Uwekezaji wa Serikali katika taasisi 10 za nje ulipanda kwa kasi, kufikia Sh1.68 trilioni kufikia Juni 30, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 98 kutoka Sh846.22 bilioni mwaka uliopita.
Ukuaji huu umetokana na mabadiliko ya viwango vya ubadilishaji wa fedha, akiba zilizokusanywa na faida za uendeshaji katika taasisi muhimu.
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Timothy Lyanga amesema kilichofanyika ni miongoni mwa mipango ya Serikali kuhakikisha mashirika yote yanachangia katika pato la taifa kupitia gawio wanalotoa.
“Na njia hii imefanya mashirika yaweze kuzalisha kwa tija na kujituma zaidi hiyo imesaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha, mianya ya rushwa na kufanya uzalishaji kuendelea kukua kila siku,” amesema.
Amesema kuendelea kufanya uwekezaji ni ishara kuwa Serikali imeridhika kuwa mashirika yanaendelea kufanya vizuri ndiyo maana inawekeza ili yaendelee kufanya vizuri.
“Kila shirika lazima litoe gawio kila mwaka kwani yalitengenezwa kutoa huduma na pia kuzalisha. Hivyo wanapoongeza uwekezaji wanachochea ukuaji wa shirika na kuyafanya kujipanua na kuongeza ajira zaidi kwa watu,” amesema.
Amesema shirika linapotanua huduma ajira zaidi zinatengenezwa na kufanya vijana waweze kuajiriwa na kuchochea uzalishaji jambo linaloenda sambamba na malengo ya serikali kuona mashirika yanakuwa na mchango mkubwa.
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Haji Semboja amesema si mashirika yote yanafanya kazi ya kutoa huduma, hivyo bali kuna mengine yanatengeneza faida hivyo uwekezaji wake lazima yatatofautiana.
“Mengine hayatakuwa na faida ila yatatoa huduma nzuri zaidi hivyo Serikali ni vyema ifikirie huduma nzuri zaidi na kutoa faida ikiwemo kuwaongezea rasilimali watu ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi,” amesema.