Pwani, Oktoba 8, 2025
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Ibrahim, ameungana na Umoja wa Wanawake wa Mkoa wa Pwani katika zoezi la usafi wa barabara ya Wilaya ya Mkuranga, Jimbo la Mkuranga, kama sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa kampeni unaotarajiwa kufanyika kesho.
Akizungumza baada ya kumaliza kushiriki usafi huo, Mariam amesema shughuli hiyo ni maandalizi ya kumpokea Mgombea Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Chimbi, ambaye anatarajiwa kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Wilaya ya Mkuranga kesho.
“Tunamkaribisha kwa moyo wa upendo na mshikamano Dkt. Emmanuel Chimbi. Ni heshima kubwa kwake kufika hapa Mkuranga kuzungumza na wananchi kuhusu dira ya maendeleo ya chama chetu,” alisema Mariam.
Aidha, amewataka wanawake na wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo muhimu, akisisitiza kuwa ni fursa ya kujifunza na kupata ufafanuzi wa sera na mipango ya chama.
“Nawaomba dada zangu, wote wa Mkuranga tujitokeze kwa wingi kesho. ni siku ya kihistoria kwa Wilaya yetu,” aliongeza Mariam.