Dar es Salaam. Tundu Lissu amehitimisha mahojiano na shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili, ambayo yaliambatana na vijembe kutoka pande zote mbili.
Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa siku mbili kuanzia jana, Oktoba 7, 2025, hadi leo Oktoba 8, amemhoji maswali ya dodoso shahidi huyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) George Bagyemu, ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu Dar es Salaam (DZCO).
Amemhoji kuhusu ushahidi alioutoa akiongozwa na mwendesha mashtaka wa upande wa Jamhuri, juu ya shtaka linalomkabili la uhaini kinyume cha kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno anayodaiwa kutamka kuhusu kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam.
Maneno yaliyoko kwenye hati ya mashtaka yanayodaiwa kutengeneza kosa la uhaini yanasomeka: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru (kiongozi wa jopo), na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Lissu ametumia muda mrefu kuelezea wasifu wake, kisha akamhoji shahidi iwapo anafahamu hivyo au hafahamu.
Shahidi katika majibu yake aliyokiri kuyafahamu, anayafahamu kwa sehemu, hayafahamu na mengine ameyakana.
Lissu katika wasifu wake amejikita katika harakati zake za kupigania demokrasia na utetezi wa haki za watu mbalimbali. Mengine yalihusu nyadhifa na tuzo alizopata ndani na nje ya nchi kutokana na harakati zake.
Kwa wasifu wake, Lissu amemhoji shahidi iwapo haoni kama kesi yake ni muhimu, yenye masilahi kwa umma kwa kuwa inamhusu mtu muhimu.
Shahidi katika majibu yake amesema haoni kama ni muhimu, akidai anamfahamu Lissu kama Mwenyekiti wa Chadema Taifa, lakini mtangulizi wake alikuwa bora zaidi.
Majibu hayo yaliibua vicheko kutoka kwa Lissu na baadhi ya waliokuwapo mahakamani kusikiliza kesi hiyo. Lissu akasema kusifiwa na Polisi wa Tanzania ni kama busu lisilokusudiwa na kwamba, Mbowe (Freeman, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema) afikishiwe taarifa kuwa amefisiwa na Polisi wa Tanzania.
Akiendelea kuzungumzia wasifu wake, Jaji Ndunguru amemwambia umekuwa mrefu, naye akajibu ni muhimu kwani anataka kuonesha kama mtu mwenye wasifu huo anaweza kuwa mhaini. Jaji Ndunguru akamsisitiza ajitahidi kuufupisha.
Sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:
Lissu: Kwenye ushahidi wako ulisema ulielekeza uchunguzi wa uhaini kwa sababu Tundu Antipasi Lissu alisema atahamasisha uasi, ni kweli au si kweli?
Lissu: Shahidi, naomba uwaeleze waheshimiwa majaji kama kwenye maelezo yako kuna mahali popote ambako umetafsiri neno uasi.
Shahidi: Lipo, naona unasoma neno mojamoja, lakini kuzuia uchaguzi ni vitisho dhidi ya Serikali.
Lissu: Nataka useme tafsiri ya neno uasi.
Shahidi: Neno mojamoja sikutoa, nilitoa yote kwa pamoja.
Lissu: Naomba uwaambie waheshimiwa majaji kama kwenye hati ya mashtaka umetoa ufafanuzi wa neno nitahamasisha uasi.
Shahidi: Ufafanuzi huo upo.
Lissu: Neno uasi umetaja mara mbili sasa katika hayo niliyoyasoma bwana ACP Msomi, kuna mahali umeandika uasi ulikuwa na maana hiyo?
Shahidi: Imeandikwa vitisho kwa Serikali.
Lissu: Lakini sijaona neno Serikali hapa?
Shahidi: Neno mojamoja halipo, lakini kimaudhui lipo.
Lissu: Waheshimiwa majaji, naomba shahidi aieleze mahakama kama ana akili timamu.
Shahidi: Nina akili timamu, ndiyo maana ni ofisa wa Polisi.
Lissu: Hata wasio na akili timamu wanaweza kupewa uofisa wa Polisi. Katika hati ya mashtaka kuna ufafanuzi wa neno uasi?
Lissu: Naomba nikusomee halafu unieleze wapi umeandika neno uasi.
Shahidi: Soma mpaka mwisho.
Shahidi: Kwenye maelezo hayo mbona unasoma nusu, soma hadi mwisho.
Lissu: Una akili timamu kweli?
Shahidi: Nina akili timamu, ndiyo maana ni ofisa wa Polisi.
Lissu: Unaweza kuwa huna akili timamu na ukawa bado ni ofisa wa Polisi.
Shahidi: Mmh! Nina akili timamu.
Lissu: Mtu akivunja sheria ya vyama vya siasa bila kutoa taarifa polisi itakuwa ni kosa la uhaini au siyo uhaini?
Shahidi: Hilo si kosa la uhaini.
Lissu: Nina Sheria namba 1 ya mwaka 2024 ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Naomba uangalie hayo makosa nimeyawekea alama; yapo sura ya 7 kwenye sheria ya uchaguzi, wasomee majaji makosa hayo anza na kosa la kwanza.
Lissu: Kati ya hayo uliyosoma kuna neno la kuzuia uchaguzi?
Lissu: Katika orodha ya makosa 25, shahidi kwenye maelezo yako una maneno ya tutakinukisha uliyatumia sana, sasa nakuuliza kuhusu hayo maneno yako. Naomba uwaeleze majaji kama ulifafanua maneno ya tutakinukisha kwelikweli.
Shahidi: Sikutafsiri neno mojamoja.
Lissu: Mmh! Kesi yangu hii, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa, hivi unafikiri kunyonga mtu ni rahisi eeh! Je, mtu akisema nitakinukisha vibaya sana, anakuwa amefanya kosa la uhaini?
Shahidi: Ndiyo, anakuwa amefanya kosa la uhaini.
Lissu: Kwa sheria ya usalama wa Taifa, kusema kuwa tutazuia uchaguzi ni kosa la uhaini?
Shahidi: Ndiyo, ni kosa la uhaini.
Lissu: Ilitokea Dodoma kwa Ramadhani Kingai?
Lissu: Sasa twende kwenye PGO (Muongozo wa Utendaji wa Jeshi la Polisi). Ni sahihi, pia haki ya kutoa mawazo hadharani na kujiunga na chama cha siasa?
Lissu: Ni sahihi na haki kwa mtu yeyote kuunda chama na kupinga Serikali iliyopo madarakani.
Shahidi: Kwa njia halali siyo kosa.
Lissu: Ni kweli au siyo kweli, katika nchi yenye vyama vingi vya siasa, kuipinga Serikali iliyopo madarakani si kosa?
Shahidi: Kama ni kwa njia halali, si kosa.
Lissu: Shahidi, kwenye PGO ni sahihi. Hii ni kesi yenye umuhimu mkubwa kwa umma?
Lissu: Hii kesi ni muhimu kisiasa?
Shahidi: Siuoni umuhimu wake.
Lissu: Wewe, huo umuhimu wa mshtakiwa kisiasa huuoni?
Lissu: Kesi hii ina umuhimu mkubwa kisiasa kwa umma?
Lissu: Kwenye hii kesi, mshtakiwa huyu ni mtu muhimu kisiasa katika nchi hii?
Lissu: Unafahamu mshtakiwa huyu amekuwa mpigania haki na mabadiliko tangu akiwa jeshini?
Lissu: Wewe ni polisi wa namna gani na umetamba jana, umesoma na una Master mbili (Shahada ya Uzamili), na sasa unasema unachukua PhD. Ni kweli kuwa kwa sasa unachukua PhD?
Shahidi: Ndiyo, nachukua PhD (Shahada ya Uzamili). Lakini usinilazimishe kuongea kitu ambacho sikijui.
Lissu: Sasa wewe ni ACP wa aina gani?
Shahidi: Na ndiyo maana nimepata cheo hiki, siyo kila mtu anapata.
Lissu: Mmh! Kwa Tanzania hii ninayoifahamu, siyo kila mtu anapata na siyo kila mtu anayepata anastahili. Waeleze majaji kama unafahamu Mei, 2011, yaani miaka 14 iliyopita mshtakiwa huyu alipata tuzo ya utendaji wa haki za mazingira.
Lissu: Waeleze majaji kama unafahamu mimi nilipata tuzo ya kupigania haki iliyotolewa na George Bush na kwamba mimi ni Mwenyekiti wa Chadema.
Shahidi: Wewe ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa na umekuwa mbunge, lakini lile suala la umuhimu naliondoa, mtangulizi wako alikuwa bora zaidi kuliko wewe.
Lissu: Kama alikuwa bora kuliko mimi, sawa. Kusifiwa na polisi wa Tanzania ni kama slip of kiss (busu lisilokusudiwa) huku akicheka. Sasa mfikishieni taarifa Mbowe huku mapolisi wanamsifia sana.
Kesi itaendelea kesho, Oktoba 9, 2025, ambapo shahidi huyo atahitimisha ushahidi wake kwa kuhojiwa na waendesha mashtaka wa Jamhuri kuhusu yaliyojitokeza wakati wa maswali ya dodoso ya Lissu.