Mageuzi kuelekea nishati safi yamechochea mabadiliko makubwa katika sera na mikakati ya kiuchumi ya nchi zinazotegemea mafuta.
Kupungua kwa utegemezi wa nishati isiyosafi duniani pamoja na shinikizo la kimataifa la kupunguza hewa ukaa, kumelazimu mataifa haya kufikiria upya vyanzo vyao vya mapato.
Nchi kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar zimeanza kuwekeza kwenye sekta mbalimbali nje ya mipaka yao ikiwamo katika nishati mbadala, kilimo, viwanda na miundombinu.
Lengo ni kuongeza wigo wa uchumi na kujihakikishia usalama wa kifedha kwa vizazi vijavyo na hiyo inaifanya Afrika kuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji kutokana na rasilimali, ukuaji wa soko na fursa za maendeleo.
Tanzania ni moja kati ya nchi inayonufaika na uwekezaji huu kwani katika robo mwaka ya Julai hadi Septemba 2025 UAE ilikuwa kinara kwa kuwekeza mtaji mkubwa kati ya nchi zote ambazo zimeonyesha nia ya kuwekeza.
UAE iliwekeza Sh1.232 trilioni kati ya Sh6.18 trilioni iliyowekezwa katika kipindi husika ikiwa imeitangulia China ambayo mara kadhaa imekuwa ikisimama kileleni katika takwimu hizo ambazo hutolewa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza).
China ikiwa nafasi ya pili, iliwekeza Sh985.805 bilioni ikifuatiwa na India iliyokuwa na mtaji wa Sh432.423 bilioni.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 06, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Tiseza, Gilead Teri alisema Tanzania inaendelea kushuhudia ongezeko la uwekezaji mpya katika mwaka 2025 licha ya nchini kuwa kipindi cha uchaguzi.
“Katika robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba tumerekodi miradi 201 yenye thamani ya Sh6.18 trilioni ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 20,808. Katika miradi hiyo viwanda iliongoza kwa kuwa na miradi 85, ujenzi wa majengo ya biashara 30, uchukuzi 29, utalii 24 na kilimo 13,” alisema.
Akiitaja mikoa iliyoongoza kwa kurekodi miradi mingi amesema Dar es Salaam iliongoza kwa kuwa na miradi 79 yenye thamani ya Sh2.03, Pwani ikiwa na miradi 29 yenye thamani ya Sh417.99 bilioni.
“Mikoa mingine ni Mwanza yenye miradi 12 ikiwa na mtaji wa Sh482.97 bilioni, Dodoma ikiwa na miradi 13 ikiwa na mtaji Sh455.32 bilioni na Arusha ikipata miradi16 yenye mtaji wa Sh261.02 bilioni,” alisema Teri.
Alisema matokeo haya yanaonyesha mwendelezo chanya wa kukua uwekezaji katika miradi mbalimbali nchi huku akiwaita Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo huku nchi za Jumuiya ya Umoja wa Kiarabu, China na India zikiwa kinara kwa kusaka fursa hizo za uwekezaji.
Ili kukuza uwekezaji zaidi na kufikia malengo yaliyowekwa katika mwaka huu wa fedha, Tiseza imekuja na kampeni maalumu ya kutangaza maeneo maalumu matano ya uwekezaji yaliyopewa kipaumbele.
Maeneo yaliyowekwa sokoni kwa kuanzia ni Bagamoyo, Kwala, eneo la Benjamin Mkapa, Buzwagi lililopo Kahama.
“Maeneo hayo yapo mengi mengine Ruvuma, Mirerani, Tanga nayo tumeyapa kipaumbele, akitokea mwekezaji ndani ya miezi 12 anaweza kuanzisha kiwanda na mamlaka utampa eneo bure,” amesema.
Katika maeneo hayo bidhaa kumi zimepewa kipaumbele ambazo wawekezaji wanaweza kuzalisha ikiwamo zile za matumizi ya haraka, bidhaa uzalishaji wa nguo, viwanda vya uzalishaji wa dawa, uunganishaji wa magari utengenezaji magari na vipuri, karatasi na vifungashio, bidhaa za mpira na raba ikiwamo matairi.
Bidhaa nyingine zilizopewa kipaumbele ni uundaji injini za boti, pikipiki, utengenezaji sola, za umeme jua, betri, teknolojia nyingine vifaa vya umeme na samani za ujenzi.
Akizungumzia suala hili, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema kwa sasa nchi za Kiarabu zinajitahidi kutawanya uchumi wao ili wasitegemee mafuta na wanatafuta njia mbadala za kujenga uchumi wao na vipato kwa wananchi wao.
“Nadhani tunapaswa kuangalia uwekezaji umeenda wapi zaidi, wamewekeza sehemu gani zaidi, kusema uwekezaji wao umeongezeka haitoshi, kwa sababu kuna nchi zimechangamka hivi karibuni ndiyo wameanza kutafuta kuwekeza katika maeneo tofauti,” amesema.
Amesema hali hiyo imewafanya waanze kuwekeza kwenye viwanda, bandari, hoteli, misitu hivyo ni mikakati ya kukuza uchumi na kujenga uchumi himilivu kupitia kujenga vyanzo vya mapato ili hata ikitokea mafuta yameisha au yamepoteza thamani wawe na namna ambavyo wanaweza kupata fedha.
“Uwekezaji wake si kwa Tanzania tu unaweza kuwa katika nchi nyingi zinazoendelea kwa sababu wanataka kuwekeza katika vitu mbadala tofauti na mafuta waliyonayo sasa,” anasema Dk Olomi.
Anasema hilo limeonekana si kwa UAE pekee bali hadi kwa nchi kama China ambayo tayari uchumi wake umekua lakini wamekuwa wakisaka vyanzo mbalimbali vya uwekezaji ikiwamo Tanzania ambazo uchumi wake unakua.
Mtaalamu mwingine wa Uchumi, Oscar Mkude amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita uwekezaji umekuwa ukitokea katika nchi ambazo hazikuwa na utamaduni wa kuwekeza.
Anasema si UAE pekee bali pia nchi kama Uturuki, Qatar, Misri nazo zinachipukia jambo ambalo linafanya watu kujiuliza kwa nini katika kipindi hiki wakati ambao namna ya uwekezaji Tanzania haujabadilika.
“Labda kitu ambacho kilikuwa kikionekana ni hofu ambayo walikuwa nayo wafanyabiashara wa nje na waliokuwapo nchini walifunga baadhi biashara zao tofauti na sasa. Hii inaweza kuwa mazingira ya uwekezaji yameongezeka lakini tunataka kuona watu kutoka mataifa mbalimbali wanakuja kuwekeza si upande mmoja,” anasema.
Nchi nyingi washirika wa zamani kama Marekani inaweza kuleta athari kubwa baadaye kwani watu wanaweza kuona kushirikiana na Marekani ni kitu cha hatari kwani Marekani wanaweza kuamua vinginevyo jambo ambalo likawaumiza.
“Hilo linaweza kufanya baadhi ya mataifa kuangalia sehemu nyingine za uwekezaji,” anasema Mkude.
Anasema uwekezaji huu ni vyema uwe katika kampuni tofauti na isiwe wa kampuni moja kwani endapo ikitokea wanataka kufunga mradi wao inaweza kuleta athari kubwa katika uchumi wa nchi.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Kamuzora yeye anasema kitu kikubwa ambacho huwa kinaangaliwa ni mazingira mazuri ya biashara ambayo yametengenezwa na nchi yanayojumuisha sheria nzuri, utawala wa kisiasa kuwa imara.
Anasema kinachoonekana ni uchumi wa kitaasisi kwa Tanzania kuendelea kukua hasa diplomasia ya kimataifa ya uchumi inapoimarishwa na viongozi wake kwa kuvuta wawekezaji kutoka nje.
“Tumeona Rais Samia Suluhu Hassan akienda Uarabuni na kuzungumzia mazingira mazuri ya biashara, hiki ni kitu cha kwanza na mengine yanafuata na watu wanapoweka mitaji wanaangalia ni kwa kiasi gani biashara zao zinaweza kustawi,” anasema.
Anasema kuwapo kwa mazingira mazuri ya kibiashara kumefanya UAE kuvutiwa zaidi kuja nchini kuwekeza katika maeneo mbalimbali hali inayoweka urahisi kuvutia mitaji mipya.
“Hata katika historia, Waarabu ndiyo walikuwa watu wa kwanza kufanya biashara Tanzania bila kujali ilikuwa wakati wa ukoloni sasa kinachohitaji ni kuwapatia mazingira mazuri ya biashara ili waweze kuendesha shughuli zao kuendana na maono yako,” anasema.
Anasema UAE inaonekana kuongoza zaidi hivi sasa huenda kutokana na yale yanayoendelea duniani ikiwamo vita ya Ukraine na Russia, sera mbalimbali ikiwamo zile za Rais Donald Trump ambazo zinaweza kufanya mitaji mingi ya Marekani isiweze kuja katika nchi za Afrika.