Katika zama ambazo dunia inakimbilia kidijitali, Tanzania nayo imeanza safari ya kujenga mifumo bunifu inayoweza kuifanya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika Afrika Mashariki.
Kupitia CargoLink, jukwaa la kisasa la usafirishaji wa mizigo lililobuniwa na kijana Mtanzania, Azizi Omary Chamani, sekta hiyo (logistics) inatarajia kupata msukumo mpya wa kuongeza ufanisi zaidi, uwazi na teknolojia.
Ubunifu huu unatazamiwa kuboresha mtiririko wa mizigo kupitia bandari za Tanzania – Dar es Salaam, Tanga na Mtwara na hivyo kuimarisha nafasi ya nchi katika ramani ya biashara ya kikanda. Kwa mfumo huu, mizigo itasafirishwa kwa gharama nafuu, muda mfupi, na uwazi zaidi, jambo litakaloongeza ushindani wa bandari zetu dhidi ya za jirani.
Mwandishi wa makala haya amezungumza na Azizi Chamani, Mkurugenzi wa kampuni ya Top Notch Company Limited na mbunifu wa CargoLink, kuhusu mradi huu ambao unaelezewa kama injini mpya ya mageuzi katika sekta ya usafirishaji nchini.
Mbali na mradi huo Chamani amezungumza kuhusu historia yake, mipango ya biashara, mazingira ya uwezekaji hapa nchini, matarajio ya kiuchumi na wito wake kwa vijana wabunifu yenye ndoto za kijasiriamali.
Swali: Kwa kifupi elezea kuhusu wewe na historia yako?
Jibu: Jina langu ni Azizi Chamani, mjasiriamali na mbunifu mwenye umri wa miaka 35, ni mzaliwa wa Bukoba, Mkoa wa Kagera. Nilizaliwa na kulelewa Bukoba mjini, lakini safari zangu za kitaaluma na kimaisha vimenipeleka katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Nina shahada ya Uzamili ya Biashara (MBA) yenye kujikita katika Usimamizi wa Teknolojia ya Blockchain kutoka Chuo Kikuu cha Guglielmo Marconi nchini Italia.
Kwa sasa ninaishi Dar es Salaam, ambako ninaongoza kampuni ya Top Notch Company Limited kampuni ya kiteknolojia ya Kitanzania inayolenga kuendesha mageuzi ya kidijitali katika sekta kuu kama vile usafirishaji, utawala bora, na ubunifu wa viwanda vya ubunifu (creative industries).
Swali: CargoLink unahusu nini, na nini kilikuchochea kuanzisha wazo hili?
Jibu: CargoLink ni jukwaa la kidijitali la usafirishaji wa mizigo lililobuniwa kuunganisha wadau wote muhimu wa sekta hii wamiliki wa mizigo, madereva, wamiliki wa malori, na mawakala wa uondoshaji mizigo kwenye mfumo mmoja unaotumia teknolojia ya kisasa.
Wazo hili lilichochewa na hali halisi ya mnyororo wa usafirishaji nchini ambapo malori mengi hurudi yakiwa matupu baada ya kushusha mizigo, jambo linalosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na uchumi kwa ujumla.
Niliona kuwa sekta hii bado inaendeshwa kwa njia za jadi licha ya Tanzania kuwa na mifumo bora ya malipo ya simu na benki. Hapo ndipo CargoLink ilipozaliwa kama jibu la kubadili mfumo wa upangaji, usafirishaji na malipo ya mizigo, sambamba na mwelekeo wa kidijitali wa dunia.
Swali: Ni suluhu gani unatarajia italetwa na uvumbuzi wako?
Jibu: CargoLink inalenga kutatua changamoto kadhaa kuu katika sekta ya usafirishaji miongoni mwake ni safari za kurudi bila mizigo kwani sasa tutajua magari yaliyopo sehemu fulani na yanayochukua uelekeo fulani zikiwa tupu, hapa tutatumia teknolojia ya akili unde (AI).
Suluhu nyingine ni ya hali iliyokuwapo ya ukosefu wa ufuatiliaji kwa kutumia GPS kufuatilia kila safari kwa muda halisi, malipo yasiyo salama au kuchelewa kwa kuanzisha malipo ya kidijitali salama na yasiyo na fedha taslimu.
Na kubwa zaidi ni kwawaleta pamoja wadau wote muhimu katika mnyororo wa uchukuzi na usafirishaji (madereva, mawakala, wamiliki wa mizigo) kwenye jukwaa moja.
Lakini zaidi ya suluhu athari kubwa ya jukwaa hilo kibiashara ni kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kasi ya utoaji. Kwa serikali, kuongeza uwazi, ufuatiliaji, na ukusanyaji bora wa mapato na kijamii, kuongeza ajira, uwazi, na sekta ya vifaa yenye kuendeshwa kwa takwimu na teknolojia.
Kwa ujumla, lengo letu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha vifaa vya kidijitali Afrika Mashariki, sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuboresha ufanisi wa biashara na kuhimiza ubunifu wa kidijitali.
Swali: Kwa sasa mradi huu umefikia hatua gani na lini huduma zitaanza rasmi kutoa huduma?
Jibu: Mpaka sasa toleo la mtandao (web platform) tayari limekamilika, na linawawezesha wamiliki wa mizigo kuweka mizigo, madereva kukubali safari, na malipo kufanyika kwa njia ya kidijitali.
Programu za simu (Android na iOS) ziko katika hatua za mwisho za maendeleo, na zinatarajiwa kuzinduliwa ndani ya miezi michache ijayo.
Kubwa zaidi hivi karibuni tumepata cheti cha kuungwa mkono (endorsement) kilichotolewa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) mazungumzo yanaendelea kati yetu na mamlaka za serikali, taasisi za udhibiti, wadau wa sekta husika, pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha tunaanza mapema iwezekanavyo.
Mazungumzo haya yanaendelea vizuri, na tupo katika hatua nzuri ya kujenga ushirikiano wa kimkakati na makubaliano rasmi ya kitaasisi, zipo kadhaa ambazo zimetupokea na tunaendelea kuzungumza na nyingine.
Cha muhimu zaidi, mradi mzima mfumo wake, huduma na chapa ya CargoLink imesajiliwa kisheria chini ya hakimiliki, haki miliki za huduma (service mark) na alama ya biashara (trademark), kuhakikisha uhalali na usalama wa chapa hii kwa muda mrefu.
Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri kwamba CargoLink siyo tena wazo tu ni suluhisho linalofanya kazi, likijiandaa kwa uzinduzi wa kitaifa ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2026.
Swali: Ni changamoto zipi kubwa ambazo umekutana nazo mpaka sasa na zipi unazitarajia?
Jibu: Kama ilivyo kwa ubunifu wowote mkubwa, changamoto ni sehemu ya safari. Zile kuu ni kama zifuatazo:
Kwanza, uelewa na mitazamo kuwashawishi wadau wakubali mageuzi ya kidijitali kwenye sekta iliyozoea mbinu za kawaida.
Pili, rasilimali fedha na miundombinu kujenga mfumo imara na unaoweza kukua inahitaji uwekezaji mkubwa.
Na tatu ni ulinganifu wa kisheria kuhakikisha kila hatua ya kidijitali inafuata sheria za nchi, hasa kwenye usafirishaji, malipo, na usalama wa data.
Hata hivyo, kila changamoto imekuwa fursa ya kujifunza. Kupitia ushirikiano wa karibu na taasisi za serikali na mashirika ya sekta, tumeweza kujenga imani na ushirikiano badala ya upinzani.
Swali: Mradi huu unahitaji uwekezaji wa kiasi gani, na chanzo chake ni kipi?
Jibu: Kwa sasa, mradi unafadhiliwa na Top Notch Company Limited, huku mazungumzo yakiendelea na wadau wa kimkakati wanaotarajiwa kuwekeza.
Kwa kiwango cha utekelezaji kamili nchini na maandalizi ya kupanua kikanda, tunakadiria uwekezaji wa takribani Dola za Kimarekani 1.5 milioni (Sh3.6 trilioni) hadi Dola 2 milioni (Sh4.9 bilioni).
Fedha hizi zitatumika kwa upanuzi wa mfumo, ununuzi wa vifaa (simu janja zenye chapa ya CargoLink zilizo na GPS na programu zilizowekwa tayari), masoko, na kuongeza nguvu kazi kwa amana ya vijana wenye uwezo wa kufanikisha mradi.
Wakati huohuo tupo katika mazungumzo na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa wanaouona uwezo mkubwa wa muda mrefu katika tunachokijenga, na tunakaribisha wengine milango ipo wazi kwa washirika wa kimkakati na wawekezaji wanaona tija katika maono yetu.
Swali: Ukiachilia mbali mradi wako, unayaonaje mazingira ya biashara changa bunifu nchini?
Jibu: Mazingira ya biashara hizo (startups) nchini yanaendelea kuboreshwa, ingawa bado kuna safari ndefu. Serikali imefanya juhudi kubwa kupitia taasisi kama TIC (sasa TISEZA) na miradi ya ubunifu chini ya COSTECH.
Hata hivyo, changamoto bado zipo hasa kwenye upatikanaji wa mitaji, mwongozo (mentorship), na fursa za kujitangaza. Kuna haja ya ushirikiano zaidi kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuharakisha uhalisia wa ubunifu unaotoka kwa vijana.
Hata hivyo, nina matumaini makubwa Tanzania ina vijana wenye akili na ubunifu mkubwa, na kadri mageuzi ya kidijitali yanavyoendelea, mustakabali wa startups nchini ni mzuri sana.
Swali: Kwa maoni yako, je, kuna nafasi na fursa kubwa za ukuaji kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) nchini kwa sasa?
Jibu: Ndiyo, kabisa. Uchumi wa Tanzania kwa sehemu kubwa unategemea biashara ndogo na za kati (SMEs) zinachangia zaidi ya 90% ya biashara zote na kutoa ajira kwa mamilioni.
Kinachohitajika sasa ni uwezeshaji wa kidijitali kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kutumia teknolojia katika biashara, masoko na fedha.
Majukwaa kama CargoLink yameundwa kwa dhumuni hilo hatulengi makampuni makubwa pekee, bali tunatoa zana zinazowawezesha wasafirishaji wadogo, wazalishaji wa ndani, na madereva binafsi kushindana kwa ufanisi katika uchumi wa kidijitali.
Swali: Ukiwa miongoni mwa wabunifu una ujumbe gani kwa vijana wa Kitanzania wenye mawazo ya ubunifu lakini wanakosa rasilimali au fursa ya kuyaendeleza?
Jibu: Ushauri wangu ni rahisi: Kwanza anza na ulicho nacho, na anza sasa. Usisubiri mazingira kuwa kamili anza kidogo, jifunze, shirikiana na wengine, na endelea kuboresha.
Pili, amini katika wazo lako na uwe na uthabiti na uthubutu. Mara nyingi, tofauti kati ya mafanikio na kushindwa ni uvumilivu.
Mwisho, kumbuka kwamba ubunifu si teknolojia pekee bali ni kuhusu kutatua matatizo halisi ya kijamii. Ukiunda suluhisho lenye thamani kwa jamii, msaada na fursa vitakuja tu vyenyewe.