Shauri kutekwa Polepole, wakili aomba kuwasilisha taarifa mpya mahakamani

Dar es Salaam. Wakili  Peter Kibatala anayeongoza jopo la mawakili wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ameomba kuwasilisha mahakamani kiapo cha ziada katika shauri la maombi ya kutekwa kwa Polepole, akidai kuwa jana na leo wamepata taarifa mpya kuhusiana na suala hilo.

Wakili Kibatala ametoa ombi hilo leo Alhamisi, Oktoba 9, 2025, wakati shauri la maombi ya amri ya mahakama ya Polepole kufikishwa mahakamani, kwa lugha ya kisheria  Harbeas Corpus lilipoitwa kwa ajili maelekezo maalumu ya mahakama.

‎Katika shauri hilo ambalo mwombaji ni Polepole,  wajibu maombi ni pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), ambaye ni mjibu maombi wa kwanza.

Wajibu maombi wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC), mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia.

Shauri hilo la maombi namba 24514/2025  linalosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fatima Maghimbi, lilifunguliwa mahakamani hapo na Wakili Kibatala kwa niaba ya Polepole, Oktoba 7, 2025, chini ya hati ya dharura.

‎‎Katika  hati hiyo ya dharura iliyothibitishwa na Wakili Kibatala anaeleza kuwa  tangu Juzi Oktoba 6, 2025, Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi  waliovamia nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

‎‎Pia, wakili Kibatala anadai kuwa mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na inaaminika kuwa amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.

‎‎”Hivyo haki zake za Kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi,” amesema Kibatala na kuongeza:

‎‎”Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake.”

‎Katika hati maombi wanaomba wasikilizwe upande mmoja na Mahakama iamuru Polepole afikishwe mahakamani akisubiri uamuzi wa maombi hayo kusikilizwa pande zote.

‎‎Katika usikilizwaji wa maombi hayo pande zote wanaomba mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamuachilie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika Mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.

‎Wakati shauri hilo lilipoitwa leo ni mjibu maombi wa pili tu DPP aliyefika mahakamani akiwakilishwa na mawakili wa Serikali Waandamizi, Faraji Nguka (kiongozi wa jopo), Debora Mushi, Edith Mauya na Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru.

‎Pamoja na mambo mengine Wakili Kibatala ameomba kuwasilisha kiapo cha ziada akidai kuwa tangu walipofungua shauri hilo juzi, kati ya jana na leo asubuhi wamepata taarifa mpya kuhusiana na suala hilo.

Ingawa mawakili wa Serikali hawakupinga kuhusiana na ombi hilo la mjibu maombi kuwasilisha kiapo cha ziada lakini kumeibuka mvutano wa kisheria katika hoja mbalimbali ambazo mahakama imepanga kuzitolea uamuzi saa 8: 00 mchana, leo.

Jinsi mambo yalivyokuwa mahakamani  

Wakili Nguka licha ya kujitambulisha kuwa anamwakilisha DPP pia ameieleza mahakama kuwa anashikilia mikoba ya mjibu maombi wa tatu, AG, ambaye pamoja na wajibu maombi wengine hawakufika mahakamani wala wawakilishi wao.

Japo amesema kuwa wao, DPP alipelekewa hati ya wito wa kufika mahakamani jana, lakini AG hakuwa amepelekewa wito huo.

Hivyo, ameiomba mahakama iwapatie muda wa kuwasilisha kiapo kinzani kujibu maombi hayo, mpaka kufikia Jumanne, juma lijalo.

” Ofisi ya DPP  ilikuwa served (ilipewa wito na nyaraka za shauri) jana na kwa asili ya maombi yalivyoletwa, ilibidi tufanye mashauriano ili kupata maelezo ya kina ya madai yalivyoletwa na mwombaji, lakini hatukuwapata wote waliotakiwa kutoa majibu hayo”, amesema Wakili Nguka na kusisitiza;

“Kwa kuwa ni haki kwa mjibu maombi kupewa nafasi ya kujibu maombi na hata wajibu maombi ambao hawakuweza kufika waweze kupewa haki hiyo.”

Amedai kuwa licha ya kwamba maombi yameletwa kwa hati ya dharura, lakini haiondoi haki ya msingi ya wajibu maombi kuleta kiapo chao cha kujibu kile kilichodaiwa na   kwa kuelewa uharaka uliopo, mpaka Jumanne tutakuwa tumejibu.”

Hata hivyo, Wakili ‎Kibatala, akisaidiana na mawakili Faraji Mangula, Alphonce Nachipiangu, Deogratius Mahinyila, na Grolia Ulomi, ameieleza mahakama kuwa wajibu maombi wote akiwemo AG wamepelekewa wito huo jana na wote walisaini na ushahidi uko katika mfumo wa mahakama.

“Kwa maoni yetu wote hawa wamekuwa served (wamepewa hati za wito), hivyo tunaomba mahakama itoe maelezo kwa hao ambao hawakufika”, amesema Kibatala.

Hivyo, ameiomba amri  ya mahakama kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo upande mmoja bila kuwepo wajibu maombi ambao hawakufika mahakamani kwa kuzingatiwa kuwa maombi hayo yamefunguliwa chini ya hati ya dharura.

Pia, Wakili Kibatala amesema kuwa DPP hawezi kumwakilisha AG na hivyo  iwekwe kwenye kumbukumbu kuwa pia hajafika mahakamani.

Katika ombi la pili, Wakili Kibatala ameomba kuwasilisha kiapo cha ziada akisema kuwa jana na leo wamepata taarifa za ziada kutoka kwa ndugu wa mwombaji ambazo zimewafikia na wamedhamiria kuziwasilisha mahakamani. 

Vilevile amesema kuwa katika maombi hayo kuna maombi ya upande mmoja ambapo mwombaji ameomba aletwe mahakamani leo hii binafsi, wakati mahakama inasubiri kusikiliza maombi haya kwa pande mbili.

“Kwa hiyo tunaomba mahakama itoe nafuu iliyoombwa kwenye  maombi ya upande mmoja, mwombaji (Polepole) aletwe mahakamani wakati tukisubiri usikilizwaji wa pande zote”, amesema Kibatala na kuongeza kuwa wamekidhi vigezo vya kikanuni kuomba amri hiyo.

Pia, ameomba kuwa baada ya DPP kuwasilisha kiapo kinzani Jumanne na wao  wanaomba Jumatano wawasilishe majibu dhidi ya kiapo kinzani, na akaomba wapangiwe tarehe ya karibu ya usikilizwaji kwa kuwa shauri  limefunguliwa  chini ya hati ya dharura.

Akijibu hoja ya mwombaji kuwasilisha kiapo kinzani, Wakili Nguka amesema kuwa ni dhahiri  taarifa mpya za mwombaji zitaisaidia mahakama kuyachambua madai hayo na akaomba mahakama iwape muda kuleta kiapo kinzani.

Pia, amedai kuwa kwa kuwa mjibu maombi wa pili ametokea mahakamani; katika mazingira hayo maombi hayo yanapaswa kusikilizwa pande  zote badala ya upande mmoja.

Wakili Nguka amedai kuwa maombi ya namna hiyo  yanapowasilishwa, sheria inamuhitaji mwombaji aieleze mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 413(1)(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) marejeo ya Mwaka 2023 aieleze mahakama huyo mtu anayetakiwa kuletwa anashikiliwa na nani kati ya wajibu maombi.

Amedai kuwa  katika shauri jambo  hilo halijaoneshwa anashikiliwa na mjibu maombi yupi. 

“Katika shauri hili ni dhahiri hakitekelezeki kwani mpaka sasa hakuna mjibu maombi ambaye tumeambiwa anamshikilia mwombaji,” amesema Nguka na kuongeza:

“Ili kuonesha kuwa mtu huyo hajulikani anashikiliwa na nani, wakili wa mwombaji katika aya ya saba ya kiapo chake anasema mtu huyo anashikiliwa na watu wasiojulikana na mahali pasipojulikana, kwa hiyo ni vigumu mahakama kutoa amri inayoombwa kwa sasa ya kuamuru aletwe.”

Amesema katika aya ya  10 ya kiapo hicho wakili  anasema kuwa anahisi kuwa anashikiliwa na mjibu maombi wa tano kwa kuwa hizo ni hisia, wanaomba mahakama isiitoe amri hiyo.

Wakijibu tena hoja hizo, Wakili Kibatala amedai kuwa  siyo kweli, kwa kuwa kuwepo kwa mjibu maombi wa pili kunaathiri usikilizwaji wa  maombi ya upande mmoja ya mwombaji kuletwa mahakamani.

“Kwa hiyo tunaomba maombi ya upande mmoja yaendelee kufanya kazi isipokuwa kama mahakama itaona vinginevyo.”

Kuhusu hoja kwamba kifungu cha 413(1)(b) hakijaonesha ni mjibu maombi gani anamshikilia mwombaji amesema kwamba  aya ya 10, inajibu hoja hiyo.

“Aya hiyo inasema nina sababu za kuamini mjibu maombi wa tano ana taarifa na anamshikilia mwombaji. Mjibu maombi wa tano ni ZPC. Sasa hapa utata uko wapi wakati imenyooka? Kwa hiyo si kweli kwamba kiapo hakijasema nani anamshikilia”, amesema Kibatala.

Jaji Maghimbi baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo mpaka saa 8 mchana huu kwa ajili ya uamuzi.