Mvutano Waibuka kati ya Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Humphrey Polepole

Shauri hilo la maombi ya amri ya kufikishwa mahakamani limefunguliwa na mawakili wa Polepole, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba yake Polepole.

Mapema leo Aprili 9, 2025 wakili Kibatala ameomba mbele ya Jaji Salma Magimbi kuwasilisha kiapo cha ziada huku akiomba Mahakama itoe uamuzi wa maombi ya upande mmoja Polepole afikishwe mahakamani ili iweze kumuona wakati akisubiri shauri la maombi yake kusikilizwa pande zote.

Wajibu maombi Katika shauri hilo lililoitwa chini ya hati ya dharura, ni, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polis Kanda Maalum Dar es Salaam (ZPC)

Kibatala aliieleza mahakama kuwa ingawa baadhi ya wajibu maombi hawakufika mahakamani, wote wamekuwa served kisheria, hivyo maombi yanaweza kuendelea hata bila wao kuwepo.

“Tumetambua kuwepo kwa DPP, lakini wengine wote hawajatokea. Wote hawa wamekuwa served na ushahidi upo mahakamani,” alisema Kibatala, akieleza kuwa hati za wito zilifikishwa kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Mwanasheria Mkuu (AG), Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Kamishna wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (ZCO) na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZPC).

Alisema IGP yuko Dodoma, lakini wito ulitumwa kupitia barua pepe rasmi ya jeshi la polisi (info.phq@tpf.go.tz) saa 5 asubuhi Oktoba 8, 2025. “Kwa amri ya mahakama kutumia teknolojia ya kisasa, tunaamini imemfikia IGP,” alisema.

Kibatala aliongeza kuwa AG na ZCO walithibitisha kupokea barua hizo, huku ZPC akipokea mara mbili

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Nguka aliiomba mahakama kuwapa muda wa hadi Jumanne ijayo ili kuwasilisha kiapo kinzani, akibainisha kuwa maombi hayo yameletwa kwa dharura na hivyo ofisi ya DPP imehitaji muda kufanya mashauriano ya kina na taasisi husika.

“Ni haki ya msingi kwa mjibu maombi kujibu maombi yaliyowasilishwa dhidi yake. Licha ya kwamba yameletwa kwa dharura, haki hiyo haiwezi kunyimwa,” alisema Nguka.

Kibatala alisisitiza kuwa tayari upande wake unakusudia kuwasilisha kiapo cha ziada kutokana na taarifa mpya zilizopatikana jana Oktoba 8 na leo asubuhi, aoktoba9,2025 akitaka mahakama iruhusu kiapo hicho kiwasilishwe leo ili mjibu maombi wa pili ajibu kwa pamoja vyote viwili.

Katika hoja zake za kisheria, Kibatala alirejea Kanuni ya III na IV ya GN 159 ya mwaka 1930 chini ya Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), akieleza kuwa maombi ya aina hii yanapaswa kusikilizwa ex-parte (upande mmoja) ikiwa mwombaji anaamini mtu anayehusika anashikiliwa kinyume cha sheria na mamlaka.

Hata hivyo, upande wa serikali ulipinga hoja hiyo, ukidai kuwa mwombaji hakubainisha ni nani hasa anayemshikilia Polepole, jambo linalofanya mahakama ishindwe kutoa amri ya kumleta mahakamani kwa sasa.

“Kiapo cha mwombaji hakioneshi wazi nani anamshikilia. kiapo kinasema anashikiliwa na watu wasiojulikana, jambo linaloleta utata. Haiwezekani mahakama kutoa amri bila kujua nani anashikilia mtu huyo,” alisema Nguka.

Kibatala alijibu akisema kiapo kinaeleza bayana kuwa mjibu maombi wa tano, yaani ZPC, ndiye anayehusishwa na kumshikilia Polepole, hivyo hakuna utata wowote.

“Aya ya 10 ya kiapo inasema nina sababu za kuamini mjibu maombi wa tano(ZPO) anamshikilia mwombaji. Kwa hiyo hoja kwamba hatujasema nani anamshikilia haina mashiko,” alisema.

Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi Jumatano ijayo, ikitoa nafasi kwa wajibu maombi kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani, huku waombaji wakiruhusiwa kuwasilisha kiapo cha ziada kabla ya siku hiyo.

Kesi hiyo itaendelea saa nane mchana kwa ajili ya kutolewa uamuzi.