Balozi wa India nchini ahimiza uwekezaji kwa vijana

Dar es Salaam. Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey amesema vijana ndiyo wanashikilia mustakabali wa Taifa lolote duniani, hivyo ni muhimu kuwapa fursa na kuwajengea uwezo katika mambo wanayoyafanya ikiwemo utamaduni.

Balozi Dey amebainisha hayo usiku wa jana katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa tuzo za uchoraji wa picha zijulikanazo kama ‘Tanzania on Canvas’ zilizowashindanisha wanafunzi katika shule za sekondari jijini Dar es Salaam.

Shindano hilo lililoandaliwa na ubalozi wa India nchini Tanzania, lilishindanisha uchoraji wa picha zinazoelezea utamaduni wa Kitanzania.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dennis Londo, Balozi Dey amesema ni muhimu kukuza fikra za vijana kwani wao ndiyo wasanifu wa mustakabali wa baadaye.

Amesema juhudi kama kuwa na “Tanzania on Canvas” ni hatua ndogo lakini muhimu katika kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Balozi huyo ameongeza kuwa ingawa biashara na uwekezaji ni muhimu, kinachodumisha urafiki huo ni uhusiano kati ya watu wao  hasa vijana wetu.  Amesema kupitia ushirikiano na shule, kuhimiza ubunifu na kujenga madaraja ya kitamaduni, wanawekeza katika mustakabali wa mataifa yao.

“Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa washirika wetu, wakuu wa shule, walimu waliojitolea, na wazazi waliounga mkono mpango huu. Lakini zaidi ya yote, nawapongeza wasanii chipukizi ambao vipaji na mawazo yao ya kiubunifu yanatupa msukumo leo,” amesema.

Amesema Tanzania sasa inashika nafasi ya pili kama mshirika wa kibiashara wa India barani Afrika, ambapo biashara imefikia Dola za Marekani 8.6 bilioni kwa mwaka 2024–25.

“Uwekezaji wa India nchini Tanzania ni miongoni mwa zilizo juu zaidi, ukifikia karibu dola 5 bilioni, kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Hii si biashara tu; ni ahadi ya muda mrefu kwa ukuaji na ustawi wa Tanzania,” amesema Balozi huyo.

Amesisitiza kwamba kujenga uwezo kumeendelea kuwa kiini cha ushirikiano wao. Amesema India inajivunia kutoa nafasi 1,000 za masomo ya muda mfupi zenye ufadhili kamili, pamoja na takriban nafasi 85 za masomo ya muda mrefu.

Londo ameupongeza Ubalozi wa India nchini Tanzania kwa kuandaa mashindano hayo kwani siyo tu yanaimarisha uhusiano baina yao, bali pia yanahifadhi utamaduni wa Kitanzania kwa kutumia sanaa ya uchoraji.

“Ushirikiano kati ya Tanzania na India umezidi kuimarika siku hadi siku na tumekuwa tukishirikiana siyo tu kwenye biashara na elimu, bali pia kwenye mambo ya kiutamaduni, ninawapongeza sana kwa hili,” amesema Londo.