Dar es Salaam. Wakati mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) ukitarajiwa kufanyika, wataalamu wamekuja na mkakati wa matumizi ya Akili Unde (AI) katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
AI ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi na ubunifu katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, masoko, mazingira na mawasiliano.
Katika kuhakikisha hilo, kwa mara ya kwanza Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza wa matumizi ya AI katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi unaofanyika Oktoba 8 na leo Oktoba 9, 2025 jijini Dar es Salaam, huku wataalamu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Korea na Brazil, wakihudhuria.
AI itatumika katika kutunza na usafi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa bayoanuai kama alivyobainisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Mazingira, Profesa Peter Msoffe katika mkutano huo.

Akifafanua zaidi, Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Gustavo Nogueira amesema teknolojia ya kisasa inaweza kusaidia kupunguza hewa ukaa, ustahimilivu na kushughulikia maeneo yaliyopata changamoto ya mabadiliko hayo.
Amesema dunia inatambua mchango wa matumizi ya AI katika kustahimili na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“AI itatumika kuchambua na kubashiri athari za mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwa ujumla katika kufanikisha hilo, lazima kuongeza vituo vya taarifa na miundombinu ya teknolojia hiyo,” ameshauri.
Akitaja faida zake, amesema inatumika katika ulinzi wa mazingira na kuchochea maendeleo. Ametoa wito kwa serikali, wadau duniani kuungana ili kuhakikisha AI sio tu kwa ajili ya matumizi yaliyozoeleka, bali pia inatumika katika ustahimilivu wa mazingira.
Mshauri wa Rais Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira, Dk Richard Muyungi amesema wanajadili namna ya kutafuta fedha, kujengewa uwezo na mwisho ni teknolojia za kisasa ambazo zimeshika kasi hivi sasa.
Dk Muyungi ambaye ni Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano Afrika (AGN), amesema pia wanaangazia tahadhari na namna ya matumizi ya AI katika kutunza mazingira.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa (UN) umeamua kuleta mkutano huo wa kwanza Tanzania, hivyo ni heshima kubwa kwa nchi
Katika hilo, vijana wana fursa ya kubuni njia mbalimbali za kiteknolojia ili kukabiliana na mabadiliko hayo.
“Lazima tuhakikishe vijana wa Tanzania wanashiriki na habari njema Tanzania ni kituo cha mafunzo ya vijana katika masuala ya mazingira baada ya kuteuliwa na Umoja wa Afrika (AU),” amesema.
Balozi wa Korea nchini Tanzania, Ahn Eun Ju amesema lazima AI itumike kusaidia kukabiliana hali ya hewa, na jinsi ya kuimarisha teknolojia na ubunifu ili kufikia uchumi wa kijani.
“Korea itafanya kazi kuelekea kutumia ubunifu wake na teknolojia kufikia changamoto za kimataifa na shida ya hali ya hewa,” amesema.
Tanzania ni miongoni mwa washiriki wa Mkutano wa COP30 utakaofanyika jijini Belem, Brazil kuanzia Novemba 10 hadi 21, 2025.