OFISA Habari wa JKT Queens, Masau Bwire, amesema klabu hiyo imeahirisha kuweka kambi Uturuki kwaajili ya maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika upande wa wanaawake itakayofanyika Algeria kuanzia Novemba 25, 2025.
Lengo la JKT Queens kutaka kuweka kambi Uturuki ni kutokana na hali ya hewa ya jiji la Istanbul kuendana na Algeria ambako yatafanyika mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Bwire amesema uongozi wa timu hiyo imeahirisha safari ya kwenda kuweka kambi Uturuki baada ya kupokea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwahitaji nyota wake 13 kujiunga na timu ya Taifa ya wanawake, Twiga Stars kwaajili ya kufuzu WAFCON dhidi ya Ethiopia. Kikosi cha Twiga Stars kinatarajiwa kuingia kambini Oktoba 13, 2025 kikijumuisha wachezaji 24.
“Uongozi wa JKT Queens ulikaa na kulichakata jambo hili baada ya kupokea barua kutoka TFF, kwasababu timu yetu ni ya kizalendo inajua umuhimu wa mafanikio ya kitaifa, iliamua kuahirisha safari usiku wa leo. Huko Uturuki hatuendi kwenye mashindano bali maandalizi, hivyo haitatuathiri,” amesema Bwire.
JKT Queens ambayo ni bingwa wa Cecafa, inaungana na timu saba kutoka kanda tofauti kukipiga ili kutafuta bingwa wa Afrika kwa wanawake, taji linalotetewa na TP Mazembe ya DR Congo.
Timu zitakazoshiriki ambazo ni mabingwa wa kanda ni TP Mazembe ikiwa ni bingwa mtetezi, Gaborone United (Botswana-COSAFA), USF AS Bamako (Mali-WAFU A), ASEC Mimosas ( Ivory Coast-WAFU B), 15 De Agosto Femenino ( Equatorial Guinea-Uniffac) na AS FAR (Morocco-UNAF).