Simba Queens yatangulia fainali Ngao ya Jamii

SIMBA Queens imetangulia fainali ya Ngao ya Jamii kwa wanawake baada ya kuitandika Mashujaa Queens mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa leo Oktoba 9, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Bao la Asha Omary dakika ya 33, liliivuruga Mashujaa Queens iliyoonekana kucheza kwa kuzuia zaidi tangu mwanzo wa mechi hiyo.

Hata hivyo Simba Queens iliendelea kushambulia lango la Mashujaa Queens, lakini wapinzani wao walikuwa imara kulinda nyavu zao sambamba na kushambulia kwa kushtukiza.

SIMB 01

Mashambulizi ya Simba Queens yalimshughulisha kipa wa Mashujaa Queens, Gelwa Yona aliyeokoa mipira ya hatari mara kadhaa. Hadi kipindi cha kwanza kinatamatika, Simba Queens ilikuwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili, timu zote ziliingia zikiwa na malengo ya kusaka bao, lakini Simba Queens ikafanikiwa dakika ya 73, baada ya Aisha Mnunka kufunga na kuzima matumaini ya Mashujaa Queens kucheza fainali ya mashindano hayo.

Licha ya timu hizo kuonyesha ushindani, lakini bado hazijawa na muunganiko mzuri huku wachezaji wakionyesha jitihada binafsi.

Hii ni mara ya tatu mashindano hayo yanachezwa ikishirikisha timu zilizomaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Wanawake. 

SIMB 02

Ushindi huo unaifanya Simba Queens kuandika rekodi ya kucheza fainali nyingine ya mashindano hayo kwa mara pili sawa na mabingwa watetezi JKT Queens ambao wote wamechukua Ngao ya Jamii mara moja.

Baada ya mechi hiyo, saa 10:00 jioni itapigwa nusu fainali nyingine ikiwakutanisha JKT Queens na Yanga Princess.

VIKOSI
Simba Queens: Zuhura Waziri, Ester Mayala, Ruth Ingosi, Zainah Nadende, Elizabeth Wambui, Asha Omary, Aisha Mnunka, Vivian Corazone, Jentrix Shikangwa, Cynthia Musungu na Z.Brice.

Mashujaa Queens: Gelwa Yona, Koku Kupanga, Sabina Mbuga, Patricia Salum, Zuhura Mlekwa, Zainabu Mohamed, Rehema Abdu, Veronica Mapunda, Tabea Aibano, Sharifa Hamidu, Veronica Gabriel.