Ridhiwan: Tuwasikilize wagombea wote, tuchague kwa busara

Mbeya.  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete amewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku akionya dhidi ya kushawishika kufanya mambo yasiyoendana na utamaduni wa taifa.

Ridhiwan amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa nafasi ya kuwasikiliza wagombea wote wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ili kupima sera na ilani bora itakayoongoza taifa kwa kipindi kijacho.

Ameyasema hayo leo Alhamisi, Oktoba 9, 2025, aliposhiriki mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika Kijiji cha Mwakwenje, Wilaya ya Mbeya, ambako mwenge huo utakagua na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.3 bilioni.

Miradi hiyo inajumuisha uwekaji jiwe la msingi la bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Imezu, mradi wa maji na kiwanda cha kuzalisha hewa tiba.

Mingine ni ujenzi wa daraja la Idiga, ugawaji wa majiko ya nishati safi kwa kaya maskini katika vijiji vya Inyala na Itewe, pamoja na uzinduzi wa klabu ya kupinga rushwa.

“Nimekuja kuangalia afya na morali ya vijana waliokabidhiwa dhamana ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru na kupongeza kiongozi wake wa mwaka huu, Ismail Ali Ussi, kwa kazi nzuri. Wizara yangu inafuatilia kwa karibu na tumeona ujumbe unavyofikishwa kwa wananchi,” amesema Ridhiwan.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda akitoa salamu za mbio  za mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 mara baada ya kupokea kutoka  Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Amesema mbio hizo zitahitimishwa Oktoba 14, 2025, katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Sokoine mkoani Mbeya, mgeni rasmi atakuwa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Ridhiwan, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa siku 139 katika halmashauri zote nchini, ukihakikisha utekelezaji wa miradi iliyozinduliwa na Rais Samia unaenda sambamba na thamani ya fedha.

Ujumbe wa Mwenge
Aidha, waziri huyo ametumia fursa hiyo kutoa salamu za ujumbe wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025, unaosisitiza kulinda amani na utulivu wa nchi.

“Watanzania wenzangu, uchaguzi ni harambee ya demokrasia ya taifa letu. Kila baada ya miaka mitano tunakwenda kupiga kura kuchagua uongozi mpya wa kutupeleka mbele. Hivyo basi, tuwasikilize wagombea wote na tupime ilani zao kabla ya kufanya maamuzi,” amesema.

Kauli ya mkuu wa wilaya
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema mbio za mwenge mwaka huu zitakagua na kuzindua miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.3 bilioni, zikiwa na kauli mbiu imemayo,  Tushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu.”

Amesema mwenge utakimbizwa umbali wa kilomita 196.1, huku miradi miwili ikiwekwa  mawe ya msingi na mingine miwili ikizinduliwa rasmi.
Wakazi wa Kata ya Inyala, Wilaya ya Mbeya, wamesema uwepo wa Mwenge wa Uhuru unasaidia kuimarisha nidhamu kwa watumishi wa serikali na kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma katika miradi ya maendeleo.

Wilaya ya Mbeya imekuwa halmashauri ya tatu kukimbizwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu, ambapo Oktoba 10, 2025 utakabidhiwa kwa Halmashauri ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe.